📌BAHATI MSANJILA
Asilimia 99 ya vyama vyote vya siasa vyenye
usajili wa kudumu nchini vimesaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2025, huku Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEEC) ikionya kuwa vyama ambavyo
havijasaini kanuni hizo vitazuiwa kushiriki uchaguzi huo.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa kanuni
hizo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Rufani Jacob Mwambegele, amesema kuwa
mchakato wa kuandaa kanuni hizo umezingatia maoni ya wadau mbalimbali, wakiwemo
wawakilishi wa vyama vya siasa.
“Kila chama cha siasa kinapaswa kusaini kanuni
hizi. Chama chochote kitakachoshindwa kufanya hivyo, hakitaruhusiwa kushiriki
katika Uchaguzi Mkuu wa 2025,” amesema Jaji Mwambegele.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi na Katibu
wa Tume hiyo, Ramadhani Kailima, amesema kuwa zoezi la kusaini kanuni hizo ni
sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya sheria mpya za uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani, zenye lengo la kudhibiti matumizi ya lugha chafu na vitendo
vinavyoweza kuvuruga uchaguzi.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa walioshiriki
hafla hiyo wamesema wamesaini kanuni hizo kwa kuwa ni hitaji la kisheria, na
wamepongeza ushirikishwaji waliopata tangu hatua za awali za uandaaji wa kanuni
hizo, hadi hatua ya mwisho ya utiaji saini.
Miongoni mwa vyama vilivyosaini kanuni hizo ni
pamoja na AAFP, ACT Wazalendo, ADA-TADEA, CCK, CHAUMA, CCM, CUF, ADC, TLP, UDP,
Demokrasia Makini, DP, SAU, NCCR Mageuzi, UMD, NLD, UPDP, na NRA.
Hata hivyo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) hakikushiriki katika zoezi hilo la utiaji saini wa Kanuni za Maadili
ya Uchaguzi.
0 Comments