📌BAHATI MSANJILA
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema
Serikali imekamilisha tathmini ya awali ya athari zitakazojitokeza kwenye
miradi iliyokuwa ikifadhiliwa na Serikali ya Marekani, ambapo sekta ya afya
imeonekana kuathirika zaidi.
Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo leo, Aprili 15,
2025, bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum
(Kagera), Neema Lugangira, aliyehoji hatua zinazochukuliwa na Serikali
kupunguza athari za mabadiliko ya sera za nje katika masuala ya fedha za
maendeleo kutoka kwa nchi zilizoendelea.
Aidha, Waziri huyo aliongeza kuwa Serikali
inaendelea kufanya tathmini katika maeneo mengine ambayo huenda yakaathirika
kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko hayo ya sera, huku ikizingatia mchango
wa mashirika na wahisani wengine wa maendeleo ambao awali waliwezeshwa na
Marekani.
Katika swali la nyongeza, Mbunge Lugangira alihoji
iwapo Serikali haioni haja ya kuondoa matumizi yasiyo ya lazima ili kuokoa
fedha ambazo zinaweza kuelekezwa kufidia upungufu wa ufadhili huo.
Akijibu, Dkt. Nchemba alisema tayari Serikali
imeanza kuchukua hatua, ikiwemo kuunda timu maalum chini ya Ofisi ya Waziri
Mkuu, ambayo ilifanya mapitio ya sekta zote, na kubaini kuwa sekta ya afya
ndiyo inayohitaji msaada wa haraka zaidi.
0 Comments