SERIKALI YAJENGA MINARA 38 YA MAWASILIANO KWA BILIONI 7.1 MKOANI KILIMANJARO



    📌BAHATI MSANJILA

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa (Mb), amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inatekeleza ujenzi wa minara 38 ya mawasiliano mkoani Kilimanjaro kwa gharama ya shilingi bilioni 7.1, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha huduma bora za mawasiliano zinafika maeneo ya vijijini.

 

Akiwa katika ziara ya kukagua upatikanaji wa huduma hizo wilayani Mwanga, Waziri Silaa alizungumza na wananchi wa Kijiji cha Karamba Ndea, Kata ya Toloha, na kueleza kuwa kati ya minara hiyo, sita inajengwa katika wilaya ya Mwanga, ikiwemo mnara unaohudumia eneo la lango la kuingilia na kutoka watalii la Ndea kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.

 

“Minara hii itasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa mawasiliano ya simu kwa wananchi na pia katika maeneo muhimu ya kitalii kama lango la Ndea,” alisema Mhe. Silaa.

 

Aidha, Waziri Silaa alieleza kuwa Serikali imekamilisha mradi wa kuboresha teknolojia ya mawasiliano kwa kuhuisha minara 468 nchini kutoka teknolojia ya kizazi cha pili (2G) kwenda teknolojia ya kizazi cha tatu (3G) na cha nne (4G), ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za intaneti kwa ufanisi zaidi.

 

Katika kukabiliana na changamoto za mawasiliano kwenye lango la Ndea na maeneo mengine, Waziri aliielekeza UCSAF kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na watoa huduma kuhakikisha ujenzi wa minara unatekelezwa haraka. Pia alisisitiza kuwa maeneo yote yenye changamoto ya mawasiliano yaliyoripotiwa na viongozi wa eneo hilo, yatatupiwa jicho kwa ufumbuzi wa haraka.

 

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Mwanahamisi Munkunda, alisema kuwa uwepo wa huduma bora za mawasiliano utachochea shughuli za maendeleo, kukuza sekta ya utalii, na kuimarisha uchumi wa kidigitali katika wilaya hiyo.

 

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Toloha, Mhe. Palesio Nalio, alishukuru Serikali kwa mradi huo na kusisitiza umuhimu wa kukamilisha miradi ya kuboresha usikivu wa redio, kwani baadhi ya wananchi wamelazimika kusikiliza redio za nchi jirani kutokana na ukosefu wa mawimbi ya redio za ndani.

 

Serikali kupitia UCSAF inatekeleza mradi wa kimkakati wa ujenzi wa minara 758 katika kata 713 zilizopo kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara. Kwa Mkoa wa Kilimanjaro, minara 38 imepangwa kujengwa ambapo hadi kufikia tarehe 9 Aprili 2025, jumla ya minara 20 ilikuwa tayari imeanza kutoa huduma.

 

Katika Wilaya ya Mwanga, minara 6 imepangwa kujengwa ambapo mitatu tayari imekamilika na ipo kazini, huku mingine mitatu ikiwa kwenye hatua mbalimbali za ujenzi. Kwa ujumla, ujenzi wa minara yote 18 iliyosalia mkoani humo unaendelea kwa kasi.








 

Post a Comment

0 Comments