WMA YASISTIZA UMUHIMU WA VIPIMO SAHIHI KATIKA MIRADI MIKUBWA YA MAENDELE


 

 


📌BAHATI MSANJILA

Katika kuhakikisha  watumiaji wa bidhaa wanapata bidhaa kwa vipimo sahihi, Wakala wa Vipimo nchini (WMA) imesema imefanikiwa kuhakiki zaidi ya asilimia 90 ya vipimo vinavyotumika nchini.

Hayo yameelezwa  jijini Dodoma na Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA Bwn. Alban Kihulla wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wakala huo kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita. 

Amesema Katika kipindi cha miaka minne, WMA imefanikiwa kuhakiki jumla ya lita 30,645,930,571 za mafuta kwa meli 546 zilizowasili nchini, kukiwana ongezeko la meli 136 mwaka 2021/22 hadi meli 174 hadi kufika Februari,2025. 

Ongezeko hilo limetokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali katika utoaji wa huduma na miundombinu ya bandari.

Aidha amesema Katika jitihada za kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji na shughuli nyingine za uchukuzi, Wakala wa Vipimo imenunuamitambo kumi na mbili (12) kwa ajili ya kuhakiki vipima mwendo kwenye vyombo vya usafiri, kati ya mitambo hiyo, mitambo 10 ni inayobebeka (portable taximeter) ambayo itasambazwa kwenye mikoa.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Alban Kihulla, amesema kuwa WMA inachangia kwa kiasi kikubwa katika miradi mikubwa ya maendeleo ili kuhakikisha vipimo sahihi vinatumika, jambo linalosaidia kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kihulla amesisitiza  kuwa WMA itaendelea kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati kama vile miradi ya maji, barabara, SGR na bwawa la Nyerere ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa vipimo sahihi na viwango vya kimataifa.

Aidha, Kihulla ameeleza kuwa katika juhudi za kuboresha huduma za afya na kuepuka madhara, WMA imejipanga kufanya uhakiki wa vipimo vinavyotumika katika sekta ya afya.

Kuhusu changamoto za ufanisi wa huduma katika ujenzi kutokana na ukosefu wa vipimo sahihi, Kihulla amaeeleza kuwa WMA inafanya kila jitihada kuhakikisha changamoto hizi zinashughulikiwa ipasavyo.





Post a Comment

0 Comments