WATAALAM WA KUDHIBITI UJANGILI WA WANYAPORI NA MAZAO YA MISITU WAKUTANA DAR

 



📌Na Mwandishi Wetu, 

Wataalamu wa kudhibiti ujangili wa Wanyamapori na mazao ya misitu kutoka nchi za Malawi, Zambia na Tanzania wamekutana Jijini Dar Es Salaam kwa lengo la kujengewa uwezo na kubadilishana uzoefu wa kudhibiti ujangili wa wanyama pori na mazao ya misitu ndani ya nchi na kwenye maeneo ya mipakani.

Akifungua mafunzo hayo Naibu Waziri wa Maliasil na Utalii, Dunstan Kitandula(Mb) amesema kuwa ushirikiano katika kudhibiti ujangili wa wanyamapori na mazao ya misitu ni jambo la msingi kwa nchi wanachama wa mkataba wa Lusaka. 

Amesisitiza kuwa unganishaji nguvu ya pamoja katika mapambano dhidi ya changamoto ya ujangiri wa wanyamapori ndani ya nchi wanachama na sehemu za mipakani haunabudi kuimarishwa hasa ikizingatiwa kuwa nchi za Tanzania, Zambia na Malawi zinaunganishwa na mifumo ikolojia ya Kasungu - Luambe na Luangwa kusini katika mpaka wa Malawi na Zambia; na halikadhalika mfumo ikolojia wa miombo ambao unapatikana kusini mwa Tanzania na mashariki ya Zambia na Malawi.

Kitandula ameongeza kuwa ili kulinda Rasilimali hizi uimarishaji wa sheria na kanuni zinazosimamia uhifadhi wa wanyamapori na misitu katika Nchi wananchama wa Mkataba wa Lusaka haunabudi kutiliwa mkazo. Katika eneo hili, amesema nchi ya Tanzania imejipambanua kuwa kinara kwa kuzifanyia mabadiliko sheria zake ili kuziongezea makali ziweze kutoa adhabu kali kwa watu wanaotiwa hatiani kwa kufanya makosa ya ujangili na biashara haramu ya usafirishaji wa wanyamapori na mazao ya misitu.

Akimkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Kikosi Kazi cha Mkataba wa Lusaka Ndugu Edward Phiri amesema serikali ya Tanzania kwa kuruhusu mafunzo hayo kufanyikia nchini Tanzania. 

 Mafunzo hayo yamehudhuriwa na maafisa wanyamapori, maafisa wa Polisi, waendesha mashtaka na maafisa wa mamlaka za mapato kutoka katika nchi za Malawi, Tanzania na Zambia.






 

Post a Comment

0 Comments