VETA YAZIDI KUCHANGIA MAENDELEO YA NCHI KUPITIA ELIMU YA UFUNDI STADI KWA VIJANA

 




📌BAHATI MSANJILA

ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendelea kushiriki kikamilifu katika kufanikisha Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2025/26 kwa kuongeza nguvukazi mahiri yenye ujuzi wa kuchangia uchumi wa nchi. 

Haya yameelezwa jijini Dodoma leo Machi 3 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Kasore amesema kuwa katika kipindi cha 2021 hadi 2024, jumla ya vijana 295,175 wamedahiliwa kwenye vyuo vya VETA kupitia kozi za muda mrefu na mfupi.

Amesema Ili kupanua wigo wa udahili wa wanafunzi, Serikali imeiwezesha VETA kuongeza idadi ya vyuo vya ufundi stadi kutoka 41 mwaka 2020 hadi 80 mwaka 2025, ongezeko la takribani asilimia 100.

Ongezeko hilo linalenga kuhakikisha kuwa VETA inachangia kikamilifu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa.

 Aidha, hadi kufikia Juni 2026, vyuo vipatavyo 65 vinatarajiwa kukamilika na kuanza kutoa mafunzo, hatua ambayo itaifanya VETA kuwa na jumla ya vyuo 145 nchini. Ongezeko hili litapelekea idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kuongezeka hadi kufikia 200,000 kwa mwaka.

Katika kuhakikisha kuwa wahitimu wa VETA wanakidhi mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia, mamlaka hiyo imehuisha mitaala 42 na kuanzisha mitaala mipya 20 katika sekta mbalimbali ikiwemo TEHAMA, michezo, umeme, magari, mitambo, kilimo, ukarimu, usafirishaji, biashara, mavazi, madini na urembo.

Katika jitihada za kuhakikisha kuwa elimu ya ufundi stadi inawafikia watu wote, VETA inashirikiana na taasisi mbalimbali kuwapa mafunzo ya ufundi stadi wafungwa walioko magerezani. 

Kasore amesema kuwa hadi sasa wafungwa zaidi ya 100 wa kiume na zaidi ya 90 wa kike kutoka magereza ya Ukonga, Morogoro na Arusha wamepatiwa mafunzo katika fani za umeme, kilimo na ufugaji.

Amesema Wamepatiwa vyeti maalum vya utambuzi wa ujuzi ambavyo vitawawezesha kutambulika rasmi mara baada ya kumaliza vifungo vyao na kujiajiri au kuajiriwa katika sekta husika.




 


Post a Comment

0 Comments