📌BAHATI MSANJILA
TUME ya Madini imeweka bayana mafanikio 12 yaliyopatikana katika
miaka minne ya serikali ya awamu ya sita ikiwemo kuimarika kwa ukusanyaji wa
maduhuli yatokanayo na rasilimali madini kutoka Shilingi Bilioni 624.61 mwaka
2021/2022 hadi kufikia Shilingi Bilioni 753.82 Mwaka 2023/2024.
Ongezeko hilo limetokana na usimamizi unaofanywa na Tume hiyo
ambapo ni sawa na asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma wakati
akieleza mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo kwa kipindi cha
Mwaka 2021/2022 hadi Februari 2025,Katibu Mtendaji wa Tume Mhandisi Ramadhan
Lwamo amesema pia katika kipindi cha kuanzia Julai, 2024 hadi Februari,
2025,wamefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi Bilioni 690.76 sawa na asilimia
69.08 ya lengo la Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Amesema Muelekeo wa Tume ni kuhakikisha kuwa ifikapo Mwaka 2025 mchango wa Sekta katika Pato la Taifa unafikia asilimia 10 au zaidi ambapo mikakati mbalimbali imeandaliwa ikiwemo kuimarisha udhibiti wa biashara haramu ya madini hususan ]utoroshaji wa madini.
Vipaumbele nane vimebainishwa na Tume hiyo ikiwemo kuimarisha mazingira ya utendaji kazi wa Tume ya Madini,kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa na kuendeleza madini muhimu na madini mkakati.
Tume ya Madini ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Madini ambayo Ilianza kutekeleza majukumu yake rasmi Aprili, 2018,lengo likiwa ni kuboresha usimamizi na udhibiti wa uzalishaji na biashara ya madini kwa kuhakikisha Sheria, Kanuni na Taratibu zote zinazoongoza shughuli za madini zinafuatwa ipasavyo ili kuongeza Pato la Taifa.
0 Comments