📌Na Mwandishi Wetu,
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umetoaa
vifaa vya TEHAMA kwa shule za umma 1,121 ikiwemo kompyuta, projekta na printa
ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi wanaosoma
shule mbalimbali za umma nchini.
Hayo yameelezwa leo jijini Dodoma na Afisa
Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda wakati akizungumza na
Waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Mfuko huo kwa Kipindi cha
miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt, Samia Suluhu
Hassan.
Mhandisi Mwasalyanda amesema, sambamba na
utekelezaji wa mradi huo, UCSAF imekuwa ikiratibu mafunzo ya TEHAMA kwa shule
ambazo zinafikishiwa vifaa hivyo ili kuwawezesha walimu kuvilewa vifaa hivyo na
kutatua matatizo madogo madogo pindi vinapopata matatizo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mwasalyanda, katika kipindi
cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan, UCSAF imefanikiwa kutoa mafunzo kwa walimu 3,798 kutoka
shule 1,791 za umma nchini, kwa kushirikiana na vyuo vikuu na taasisi za elimu
nchini, ikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Taasisi ya Teknolojia Dar es
Salaam (DIT), na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Kwa upande mwingine, Mhandisi Mwasalyanda amesema
UCSAF imeendelea kuhamasisha matumizi ya TEHAMA kwa wasichana, kupitia
maadhimisho ya Siku ya Wasichana na TEHAMA, ambapo mafunzo yanatolewa kwa
wanafunzi wa kike ili kuwaandaa kwa masomo ya sayansi na teknolojia.
Katika kipindi cha Awamu ya sita chini ya Mhe.
Rais Dr. Samia Suluhu Hassan, UCSAF imetoa mafunzo kwa wanafunzi takribani 490
kutoka shule 304. Kwa mwaka wa Fedha 2024/25 wanafunzi wa kike wapatao 248
wanatarajiwa kuhudhuria mafunzo haya.
Utekelezaji huu wa UCSAF ni sehemu ya juhudi za
Serikali katika kuboresha elimu nchini, huku ikiendelea kutoa kipaumbele kwa
maeneo ya TEHAMA na masomo ya sayansi na teknolojia, ili kuendana na mabadiliko
ya haraka ya kiteknolojia duniani.
0 Comments