📌BAHATI MSANJILA
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeendelea
kuimarisha miundombinu ya kidigitali nchini, ambapo hadi sasa vijiji 1,407
katika kata 713 kwenye wilaya 127 za mikoa 26 ya Tanzania Bara vimenufaika na
mradi huo, huku wananchi milioni 8.5 wakitarajiwa kufikiwa na huduma hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma,
Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda, amesema utekelezaji
wa mradi huu umewezeshwa na ruzuku ya shilingi bilioni 126 iliyotolewa na Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kusaidia watoa huduma za mawasiliano kueneza
mtandao vijijini.
Kwa mujibu wa Mwasalyanda, hadi kufikia Mei 2025,
jumla ya minara 758 itakuwa imejengwa, ambapo minara 430 tayari inatoa huduma
kwa wananchi. Aidha, ruzuku ya shilingi bilioni 5.5 imetolewa ili kuongeza
nguvu katika ujenzi wa minara mingine 304.
Katika jitihada za kukuza ushiriki wa mabinti kwenye
masomo ya sayansi na TEHAMA, UCSAF imeanzisha programu maalum ya Msichana na
TEHAMA.
Mpaka sasa, walimu 1,585 wamepewa mafunzo maalum,
huku wasichana 1,204 wakishiriki mafunzo mbalimbali ya TEHAMA ili kuwajengea
uwezo wa kushiriki kikamilifu katika sekta ya teknolojia.
Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali,
amesema kuwa hadi kufikia Machi 27, 2025, taasisi 35 tayari zimewasilisha
taarifa za mafanikio yao kwa kipindi cha miaka minne.
Mafanikio haya yanatokana na maono na dhamira ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan kupitia slogan yake ya 4R.
Aidha, Msigwa Ameeleza kuwa kuanzia Aprili 14, 2025,
mawaziri wa wizara mbalimbali wataanza kuwasilisha mafanikio ya sekta zao kwa
umma.
0 Comments