UCHAFUZI WA ZIWA VICTORIA WAZUA ATHARI



        📌BAHATI MSANJILA

Ripoti ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imebaini kuwa utiririshaji wa maji taka kutoka viwandani, shughuli za madini, na taka za makazi ni vyanzo vikuu vya uchafuzi wa ziwa Victoria.

Madhara yaliyobainika ni kuziba kwa injini za vivuko kutokana na kuenea kwa gugu maji jipya, kuharibika kwa miundombinu, na kuathirika kwa uwekezaji katika kilimo cha samaki. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Semesi, amesema gugu maji hilo aina ya Salvinia SPPlina uwezo wa kuzaliana zaidi ya mara mbili au tatu kila baada ya siku nane na linaathiri vivuko pamoja na uwekezaji wa vizimba vya samaki katika ziwa hilo.

Amesema Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), chini ya utaratibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, wiki mbili zilizopita limezikutanisha sekta 12 ambazo zinakuja na mikakati ya kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo kutumia wavuvi ili kuliondoa kwa muda mfupi.

Katika juhudi za kupambana na uchafuzi wa mazingira, NEMC imeendelea kudhibiti matumizi ya vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango. Zaidi ya tani 150za plastiki haramu zimekamatwa na kuteketezwa kwa mujibu wa sheria. Hatua hii inalenga kupunguza athari za plastiki katika mazingira, huku wananchi wakihimizwa kutumia vifungashio mbadala vinavyooza kwa urahisi na visivyo na madhara kwa mazingira.

Pamoja na hayo, Baraza limepokea na kushughulikia malalamiko 1,483 yanayohusu kelele na mitetemo katika maeneo mbalimbali. Kelele zinazidi kuwa tatizo, hasa katika maeneo ya makazi, biashara, na viwanda, ambapo zinaathiri afya ya wananchi. 

NEMC imefanya kaguzi zaidi ya 9,600 ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele, huku kampeni za uhamasishaji zikiendelea kufanyika ili kuhakikisha sheria za mazingira zinafuatwa.

 



Post a Comment

0 Comments