TRA YAVUKA MALENGO YA MAKUSANYO


📌
BAHATI MSANJILA

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kuvuka malengo yake ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2024/25, baada ya kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 21.20 kwa kipindi cha miezi nane, kuanzia Julai 2024 hadi Februari 2025.

Hii ni sawa na ufanisi wa asilimia 104 ya lengo la shilingi trilioni 20.42, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita.

Akizungumza jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema mafanikio haya yametokana na utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyesisitiza umuhimu wa ukusanyaji wa mapato kwa weledi, upanuzi wa wigo wa kodi, na kujenga mahusiano bora na walipakodi.

Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Mhe. Rais, makusanyo ya kodi yameongezeka kwa asilimia 78, kutoka shilingi trilioni 11.92 mwaka 2021 hadi shilingi trilioni 21.20 mwaka huu. Hili ni dhihirisho la ufanisi wa juhudi za Serikali katika kuimarisha mifumo ya kodi na kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari

Bw. Mwenda.

Mwenda amesema Katika kuhakikisha mazingira bora ya biashara, TRA imeimarisha ushirikiano na wafanyabiashara kwa kufanya vikao vya mara kwa mara, kutatua changamoto zao, na kuanzisha utaratibu wa Alhamisi ya kila wiki kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya walipakodi katika ofisi zote za TRA nchini.

Pia, mamlaka hiyo imeanzisha ushirikiano na viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, na makundi mbalimbali ya kijamii ili kuimarisha uwazi katika usimamizi wa kodi.

Ameongeza kuwa TRA imeendelea kuboresha mifumo yake ya kidijitali kwa lengo la kurahisisha ulipaji kodi na kuzuia mianya ya ukwepaji kodi. 

Baadhi ya mifumo iliyoanzishwa ni pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS), Mfumo wa Forodha (TANCIS), na Mfumo wa Dirisha Moja la Kielektroniki (TeSWS), ambayo yote yamechangia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu, TRA imejiwekea mikakati ya kuendelea kuvuka malengo yake, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, kuongeza elimu kwa walipakodi, na kuimarisha uwajibikaji wa ndani kwa watumishi wake.

Bw. Mwenda amehitimisha kwa kutoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi wote kulipa kodi kwa wakati, akisisitiza kuwa “Hakuna anayeweza kukusaidia kutokulipa kodi halali, atakusaidia  akuihairisha tu, lakini mwishowe utalipa pamoja na riba na adhabu.”

Awali akizungumza katika mkutano huo Msemaji mkuu wa serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari maelezo Gerson Msigwa ametoa wito kwa wananchi kuwa wazalendo kwakulipa kodi ili kodi hiyo itumike kwenye maendeleo ya nchi









Post a Comment

0 Comments