TIB KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TAASISI ZA FEDHA KUKUZA UWEKEZAJI

 


  📌Na Mwandishi Wetu

Benki ya Maendeleo (TIB) imesema itaendelea kushirikiana na taasisi za fedha za kimataifa ili kupata mikopo ya riba nafuu kwa ajili ya kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo yenye athari chanya kwa jamii na uchumi wa taifa. 

Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Lilian Mbassy, amesema hatua hii ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kusaidia juhudi za serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa.

Mbassy ameeleza kuwa kupitia mradi wa upanuzi wa nishati vijijini, benki itaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kutoa mikopo kwa wazalishaji wa nishati jadidifu. 

Lengo ni kuhakikisha maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme wa TANESCO yanapata huduma hiyo kwa gharama nafuu, hivyo kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa Mbassy, TIB imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 630.3 katika miradi ya maendeleo hadi kufikia Desemba 2024. 

Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 408.3 zipo kwenye mizania ya benki, huku mifuko tisa inayosimamiwa na benki hiyo ikichangia uwekezaji wa shilingi bilioni 222. Uwekezaji huu umechangia kuzalisha ajira zaidi ya 12,547 katika sekta mbalimbali.

Maeneo yaliyonufaika na uwekezaji wa benki hiyo ni pamoja na sekta ya kilimo na usalama wa chakula (shilingi bilioni 162.7), elimu (shilingi bilioni 4.3), maji safi na usafi wa mazingira (shilingi bilioni 22.4), nishati safi na nafuu (shilingi bilioni 11.5), pamoja na ukuaji wa uchumi na ajira (shilingi bilioni 250.7). 

Sekta za utalii, viwanda, usafirishaji, makazi na maendeleo ya miji pia zimehusishwa katika uwekezaji huo, ambao unalenga kuongeza kasi ya maendeleo nchini.





Post a Comment

0 Comments