📌BAHATI MSANJILA
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza bidhaa zisizokidhi viwango vyenye thamani ya Shilingi bilioni 1.5 kati ya Julai na Desemba 2024, ikiwa ni hatua ya kulinda afya na usalama wa watumiaji.
Akizungumza jijini Dodoma, Mkurugenzi
Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema bidhaa hizo zilikuwa na kasoro kama
viambato hatarishi, ubora duni, na kuingizwa nchini bila kufuata taratibu za
kisheria.
Amefafanua kuwa bidhaa zilizoteketezwa ni pamoja na vipodozi vyenye viambato vilivyopigwa marufuku, chakula kilichoisha muda wake, vifaa vya umeme visivyokidhi viwango, pamoja na bidhaa nyingine zisizo na usajili wa ubora kutoka TBS.
Kwa mujibu wa TBS, shirika hilo limeendelea kuimarisha mifumo yake ya ukaguzi wa bidhaa zinazoingia nchini, ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia za kisasa katika maabara zake 12 ambazo zote zimepata ithibati ya kimataifa. Dkt. Katunzi aliongeza kuwa hatua hii imewezesha kubaini kwa haraka bidhaa hafifu na kuzuia zisifike kwa watumiaji.
Mbali na ukaguzi wa bidhaa zinazoingizwa nchini, TBS pia imeendelea kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa ndani ili kuhakikisha wanazalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, shirika hilo limeandaa viwango 1,823 vya sekta mbalimbali na kutoa vyeti na leseni za ubora 2,402 kwa wazalishaji, wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,066.
Kuhusu uamuzi wa serikali kuondoa vinywaji vidogo vya pombe kali vyenye ujazo wa mililita 50, Dkt.aQnq kuwa hatua hiyo haikutokana na ukosefu wa ubora wa bidhaa hizo, bali ni sehemu ya jitihada za serikali kudhibiti matumizi holela ya pombe kwa kuzuia upatikanaji wake kwa urahisi.
Kwa upande wa wananchi, Dkt. Katunzi amewataka kuwa makini wanaponunua bidhaa kwa kuhakikisha zinakuwa na alama ya ubora ya TBS na kuepuka bidhaa zisizo na usajili wa shirika hilo. Pia alihimiza wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapobaini bidhaa zisizokidhi viwango zikiuzwa sokoni.
0 Comments