📌Na Mwandishi Wetu,
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)
umepata mafanikio ya kuimarisha upitikaji wa miundombinu ya barabara za wilaya
wenye urefu wa kilometa 144,429.77 kwa asilimia 55 ambapo lengo ni kufikia
asilimia 60 ifikapo mwezi Juni, 2025.
Mafanikio haya yanatokana na ongezeko kubwa la
bajeti ya Wakala kutoka shilingi bilioni 275 hadi shilingi bilioni 870.3 sawa
na ongezeko la asilimia 216 kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2024/25.
Hayo yameelezwa Jijini Dar es Salaam na Mwakilishi
wa Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo ambaye pia ni Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es
Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga katika semina iliyoandaliwa na TARURA kwaajili
ya Wahariri wa Vyombo vya Habari.
Aidha, amesema katika ujenzi wa barabara
zinazosimamiwa na Wakala wameendelea kufanya majaribio kwa kutumia teknolojia
mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ya mawe 'cobble stone roads' na madaraja
ya mawe 'stone arch bridges' pamoja na teknolojia nyingine katika kuboresha
barabara wanazozisimamia.
Ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia na malighafi
za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo
ya barabara, huongeza ufanisi, huokoa muda, hutunza mazingira kwa gharama nafuu.
Hata hivyo Wakala umeendelea na matumizi ya
malighafi za ujenzi wa barabara zinazopatikana maeneo ya kazi na utafiti wa
teknolojia mbadala za ECOROADS, Ecozyme, na GeoPolymer kwenye ujenzi wa
barabara kwa lengo la kupata ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji
na kulinda mazingira, amesema Mhandisi Mkinga.
Amesema jumla ya madaraja ya mawe 350 yamejengwa
ambapo gharama zimepungua kwa kiasi cha Shilingi bilioni 10. Kwa upande wa
majaribio ya teknolojia mbadala Km. 7.95 zimekamilika na Km. 53.76 zipo kwenye
hatua mbalimbali za utekelezaji na ufuatiliaji wa ubora wa teknolojia hizo
unaendelea.
0 Comments