TANZANIA YAMTAMBULISHA PROF. MOHAMED JANABI KAMA MGOMBEA WA UKURUGENZI WA WHO KANDA YA AFRIKA

 



 

📌Na Mwandishi Wetu


 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemtambulisha rasmi Prof. Mohamed Yakub Janabi kama mgombea wake wa nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Mei 18, 2025, jijini Geneva, Uswisi.

 

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma Waziri wa Afya Jenista Mhagama amesema Tanzania inakwenda kwenye uchaguzi huu ikiwa na matumaini makubwa ya ushindi, ikiegemea diplomasia imara na sifa za Prof. Janabi katika kuleta mageuzi kwenye sekta ya afya.

 

Prof. Janabi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya na Lishe, ana uzoefu mkubwa katika sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuiongoza Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

 

Katika uchaguzi huu, Prof. Janabi atachuana na wagombea kutoka Togo, Ivory Coast, na Guinea Conakry.

 

Katika hatua nyingjne Jenista ametoa wito kwa Watanzania na wadau wa afya kumuunga mkono mgombea wa Tanzania kwa kampeni za kidiplomasia na dua.

 

Tanzania ilishinda nafasi ya Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika Agosti 2024 kupitia Marehemu Dkt. Faustine Ndugulile, lakini kabla ya kuanza majukumu yake, alifariki dunia Novemba 27, 2024. Kufuatia pengo hilo, Tanzania imemteua Prof. Mohamed Janabi kuwania nafasi hiyo ili kuendeleza mchango wa nchi katika kuboresha afya barani Afrika.

 

Serikali ya Tanzania, kwa kutambua umuhimu wa nafasi hii, imefanya maamuzi ya haraka kwa kumteua Prof. Mohamed Janabi, mtaalamu mashuhuri wa afya na kiongozi mwenye uzoefu mkubwa, kuendelea na harakati za kuwania nafasi hiyo ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kushikilia nafasi yake ndani ya WHO.

 

Prof. Janabi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ambapo alifanya mageuzi makubwa yaliyosaidia kupunguza rufaa za wagonjwa wa moyo kwenda nje ya nchi kwa zaidi ya asilimia 95.

 

Aidha, kama Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya na Lishe, amechangia kwa kiasi kikubwa katika uboreshaji wa huduma za afya nchini Tanzania na Barani Afrika kwa ujumla.

 

Prof. Janabi pia amehusika katika tafiti mbalimbali za afya za kitaifa na kimataifa, amekuwa mhadhiri wa tiba katika Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS) na mshauri wa masuala ya afya katika mashirika ya kimataifa.

 

Katika uchaguzi huu, Prof. Janabi atachuana na wagombea kutoka Togo, Ivory Coast, na Guinea Conakry.

 

Tanzania sasa inaelekeza nguvu zake katika kampeni za mwisho kuelekea uchaguzi wa Mei 18, 2025, huku ikiendelea kushirikiana na mataifa mengine ili kuhakikisha ushindi wa Prof. Janabi.

 

Post a Comment

0 Comments