TANZANIA, BARBADOS KUIMARISHA USHIRIKIANO


 



📌Na Mwandishi Wetu,


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Mottley ambapo wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Mazungumzo hayo yamefanyika  katika makazi rasmi ya Waziri Mkuu, Mia Mottley, Jijini Bridgestone, nchini Barbados.

Waziri Mkuu Mia amesema, kuna umuhimu wa kuwa na mkakati wa pamoja na kushirikiana kwa lengo la kukuza utalii kati ya Barbados na Tanzania na nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla.

Amesema kuna maeneo mengi ya vivutio vya utalii ambavyo vinaweza kuzinufaisha pande hizo mbili yakiwemo masuala ya ukarimu.

Maeneo mengine ya ushirikiano ni katika utoaji wa mafunzo maeneo ya ufundi kati ya nchi za Carib (Caribbean) na nchi mbalimbali za kiafrika huku akisisitiza kuwa umuhimu wa uboreshaji wa masoko na kubadilishana wataalam katika sekta mbalimbali kwa makubaliano maalum.

Aidha, amesema upo uhitaji wa wataalam katika sekta ya maji na miundombinu na hivyo kuna uwezekano wa kubadilishana wataalam ili kujengeana uzoefu katika sekta mbalimbali kulingana na makubaliano yatakayofikiwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Biteko amesema mapendekezo hayo ni mazuri na yanaweza kuwa matokeo chanya baada ya kuchambuliwa na watalaam katika sekta husika kupitia Wizara zinazohusika na masuala ya kidiplomasia.

Dkt. Biteko amesema Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendeleza kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo inalenga kuwawezesha asilimia 80 ya watumiaji wa nishati kuondokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi ifikapo mwaka 2034.

Katika utekelezaji wa mpango huo, amesema Tanzania inatembea kifua mbele kunadi mkakati huo wa miaka 10 ambao pamoja na mambo mengine unakusudia kupunguza madhara kwa watumiaji wa nishati isiyokuwa safi inayopelekea uchafuzi wa mazingira, magonjwa ya kupumua pamoja na vifo.

Dkt. Biteko amefafanua kuwa, hatua ya Tanzania kushiriki katika mkutano wa nishati endelevu kwa wote (SEforALL) uliofanyika nchini Barbados, ni kuthibitisha nia yake thabiti inayolenga matokeo chanya. Hivyo, amesema yapo maeneo mengi ya kushirikiana na kuwezesha wananchi wa pande zote mbili kupata maendeleo na ustawi wa pamoja.

Mkutano wa Dkt. Biteko Waziri Mkuu wa Barbados, umehitimisha ziara ya kikazi nchini humo ambako alishiriki katika Kongamano la kimataifa la nishati endelevu kwa wote pamoja na mikutano ya wadau mbalimbali iliyojikita katika uboreshaji wa sekta ya nishati kwa manufaa ya nchi hizo mbili.





Post a Comment

0 Comments