📌Na Mwandishi
Wetu,
KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kiasi cha Shilingi Bilioni 25 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR-Tanzania) ulioanza mwaka 2021-2025 katika Mikoa mitano na Halmashauri za Wilaya saba nchini.
Aidha kutokana na mwitikio
chanya wa wananchi katika kutekeleza mradi huo, Serikali imekusudia kuongeza
maeneo ya utekelezaji, katika Mikoa na Halmashauri nyingine nchini.
Mhandisi Luhemeja amesema
hayo jana Jumamosi Machi 15, 2025 Jijini Mbeya wakati akizungumza na waandishi
wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati tendaji ya kitaifa ya
usimamizi wa mradi huo kilichojadili shughuli mbalimbali za utekelezaji wa mradi
huo hadi kufikia sasa.
Luhemeja amesema tathimini
iliyofanywa na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeonesha wananchi
wamefurahishwa na utekelezaji wa shughuli za mradi na hivyo Serikali imepanga
kuhakikisha kuwa inaongeza wigo wa maeneo ya utekelezaji wake ili kuleta
manufaa katika masuala ya uhifadhi wa mazingira nchni.
Ameongeza kuwa mradi wa SLR
ni mojawapo ya miradi ya mfano ambayo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais
imekusudia kuianzisha katika maeneo mbalimbali nchini, ili kuisaidia jamii
kuongeza hamasa ya uhifadhi wa mazingira na hivyo kuweza kutumia vyema fursa ya
mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya kuibua miradi ya kijamii.
Amefafanua kuwa Ofisi ya
Makamu wa Rais itaendelea kujenga uwezo kwa jamii zinazotekeleza mradi huo
ziweze kuhamasisha katika masuala ya uhifadhi wa mazingira na
kutumia fursa zilizopo kuweza kujiongeza kipato kupitia shughuli za uzalishaji
mali.
Akitolea mfano, amesema
kupitia mradi wa SLR wananchi wameweza kutumia mbinu za kisasa za uzalishaji
mali ikiwemo kilimo rafiki kwa mazingira ambacho kimewazesha kuvuna kiasi
kikubwa cha mazao kwa kutumia mbinu za kisasa ikiwemo mbegu bora na teknolojia
ya umwagiliaji.
Aidha Luhemeja amezihimza
jamii zilizonufaika na mradi huo kutumia vyema rasilimali zilizopo ili kuwa
endelevu sambamba na kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii kutunza na
kuhifadhi mazingira kwani.
Kwa upande wake Mratibu wa
Kitaifa wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai
Tanzania (SLR), Dkt. Damas Mapunda amesema kwa mwaka 2025, mradi huo umetenga
kiasi cha Shilingi Bilioni 9.9 kwa ajili utekelezaji wa shughuli mbalimbali za
mradi.
Ameongeza kuwa hadi kufikia
sasa mradi huo umefikia asilimia 67 ya utekelezaji wake na kuongeza kuwa
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kukamilisha mradi huo
unakamilika kwa wakati na viwango vilivyokusudiwa.
Mradi wa SLR
unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira
la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mradi huo
ulianza kutekelezwa mwaka 2021 na unatarajia kukamilika mwaka 2025 na
ambapo jumla ya Mikoa 05, Halmashauri 07, Kata 18 na vijiji 54 zinatarajia
kunufaika. Halmashauri hizo ni Iringa Vijijini, Mbeya, Wanging’ombe, Mbarali,
Sumbawanga Vijijini, Tanganyika na Mpimbwe.
0 Comments