📌BAHATI MSANJILA
Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa
Madini (GST) imeanza ujenzi wa maabara ya kisasa jijini Dodoma kwa lengo la
kuimarisha uchunguzi wa sampuli za madini na kuchochea ukuaji wa sekta hiyo.
Ujenzi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali ya
Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya
madini nchini.
Akizungumza na waandishi wa Habari Kaimu Mtendaji
Mkuu na Mkurugenzi wa Huduma za Maabara wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa
Madini (GST), Notkka Banteze, amesema wanajenga maabara ya kisasa na Maabara
hiyo itakuwa na vifaa vya kisasa vitakavyowezesha uchunguzi wa madini mbalimbali,
Ametaja uchunguzi wa madini utahusisha madini ya
kimkakati kama vile kinywe (graphite), shaba, nickel, na madini tembo (heavy
mineral sands).
Amesema Kwa mara ya kwanza, wachimbaji wadogo
wataweza kupata huduma za uchunguzi wa sampuli kwa haraka zaidi, hivyo
kupunguza gharama na muda wa kusubiri matokeo.
Ameongeza kuwa Katika kipindi cha miaka minne ya
uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, GST imeshuhudia ongezeko la bajeti
kutoka shilingi bilioni 10 mwaka 2021/2022 hadi bilioni 110 mwaka 2024/2025,
sawa na ongezeko la asilimia 1,000.
Fedha hizi zimewezesha taasisi hiyo kuimarisha
tafiti za madini, kuajiri wataalamu zaidi, na kununua vifaa vya kisasa kama
mashine za mionzi za XRD na XRF kwa ajili ya uchunguzi wa sampuli za miamba na
udongo.
Sambamba na ujenzi wa maabara, Serikali
inatekeleza mradi wa kusogeza huduma za GST karibu na wachimbaji kwa kujenga
ofisi na maabara mpya katika mikoa ya Geita na Mbeya. Maabara hizi zitawasaidia
wachimbaji wadogo kufanya uchunguzi wa madini yao kwa uhakika zaidi na kuongeza
tija katika shughuli zao.
Kwa upande wa tafiti za madini, GST imekamilisha
utafiti wa jiolojia na jiokemia katika mikoa mbalimbali, ambapo matokeo
yanaonesha uwepo wa madini ya dhahabu, urani, kaolin, chokaa, na metali adimu
kama rare earth elements.
Pia, utafiti wa madini ya helium umefanyika katika
mikoa ya Arusha, Manyara, Dodoma, Singida na Shinyanga, huku matokeo ya awali
yakiashiria uwezekano wa hifadhi kubwa ya gesi hiyo muhimu kwa matumizi ya
viwandani na tiba.
Katika kuboresha mifumo ya usimamizi wa sekta ya
madini, Serikali inakamilisha ujenzi wa Kanzidata ya Taifa ya taarifa za
madini, mfumo ambao utasaidia kuhifadhi na kusambaza taarifa muhimu kwa
wawekezaji na wadau wa sekta hiyo. Hii ni hatua muhimu katika kuvutia uwekezaji
na kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa.
Amesema Mafanikio hayo yamewezekana kutokana na
uwekezaji mkubwa wa Serikali, usimamizi thabiti wa Wizara ya Madini, na
jitihada za GST katika kuimarisha utendaji wake.
0 Comments