📌BAHATI MSANJILA
Shirika la Reli Tanzania (TRC) linatarajia kuanza rasmi safari
za mizigo kupitia Reli ya Kisasa (SGR) kati ya Mei na Juni mwaka huu, Hii ni
baada ya kupokea mabehewa 264 kati ya 1,430 yaliyoagizwa kwa ajili ya kuboresha
usafirishaji wa mizigo na kuimarisha uchumi wa taifa.
Akizungumza jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja
Kadogosa, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk.
Samia Suluhu Hassan, ambaye amewekeza zaidi ya shilingi trilioni 30 katika
ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya reli nchini.
Tangu kuanza kwa safari za abiria kupitia SGR kati ya Dar es
Salaam na Dodoma, zaidi ya abiria milioni 2.1 wamesafiri, huku
mapato ya shilingi bilioni 59 yakikusanywa. Kadogosa alieleza
kuwa kwa sasa TRC inasafirisha abiria kati ya 6,000 hadi 7,000 kwa siku,
hali inayoonyesha muitikio mkubwa kutoka kwa wananchi.
Aidha amesema serikali ipo katika mchakato wa kuanza
ujenzi wa reli ya SGR Kanda ya Kusini, ambapo kwa sasa inaendelea kutafuta
fedha kwa ajili ya mradi huo.
Reli hiyo inatarajiwa kuunganisha Tanzania na nchi
za Malawi na Msumbiji, hatua itakayoongeza fursa za biashara na
usafirishaji wa mizigo katika ukanda huo.
Kadogosa amebainisha kuwa TRC imeagiza jumla ya mabehewa
1,430, ambapo mabehewa 264 tayari yamewasili na Kwa sasa,
shirika linaendelea kukamilisha taratibu mbalimbali za kiutendaji ili
kuhakikisha safari za mizigo zinaanza rasmi kati ya Mei na Juni mwaka
huu.
Amesema kuwa treni ya mizigo kupitia SGR itakuwa na uwezo
wa kubeba tani 120 kwa safari moja, kiwango ambacho ni mara tatu ya
uwezo wa treni ya kawaida, jambo litakalorahisisha usafirishaji wa bidhaa ndani
na nje ya nchi.
Kadogosa amefafanua kuwa mpango wa serikali ni kuendelea kupanua
mtandao wa reli, ambapo ifikapo mwaka 2027, SGR inatarajiwa
kufika Mwanza, na ifikapo mwaka 2028, itakuwa
imefika Kigoma.
Aidha, serikali inaendelea na
mkakati wa kuunganisha reli ya SGR hadi Burundi, hatua
itakayowezesha Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji wa mizigo kwa nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC).
Kuanzishwa kwa safari za mizigo
kupitia SGR ni hatua muhimu kwa uchumi wa Tanzania, kwani kutapunguza gharama
za usafirishaji wa bidhaa, kuongeza ufanisi wa biashara, na kuimarisha
ushirikiano wa kikanda.
0 Comments