RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,
ametoa maagizo kwa wale wote waliobainika kuhusika na upotevu wa mapato
wachukuliwe hatua kali mara moja huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi thabiti
wa fedha za umma kama nyenzo kuu ya kuimarisha mifumo ya serikali na kuleta
maendeleo endelevu.
Akizungumza katika mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Rais Samia ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa inayoikabili serikali ni ukusanyaji na matumizi ya mapato, ambapo bado kuna watu wanaendesha mifumo isiyo halali ya ukusanyaji wa fedha katika halmashauri, hali inayosababisha upotevu wa mapato.
Amefafanua kuwa mifumo hiyo ya pembeni imekuwa ikikusanya fedha ambazo hazifikii mifumo rasmi ya serikali, badala yake zinaishia mikononi mwa watu binafsi.
Awali Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amesema maendeleo siyo ahadi bali ni hatua zinazochukuliwa Kila siku huku akisema kauli hiyo inayohusisha utekelezaji wa vitendo katika mchakato wa maendeleo.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Murshid Ngeze amesema Wiki ya Serikali za Mitaa itaziwezesha Serikali za Mitaa kupitia halmashauri zake kuonesha miradi ambayo imetekelezwa kupitia mapato ya ndani ili wananchi wajue nini Serikali yao inafanya kupitia mapato inayoyakusanya.
Ikumbukwe kuwa Benki ya NMB katika kuimarisha mahusiano mazuri na Jumuiya hiyo imedhamini mkutano huo kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 170 ikiwa ni mwaka wa tisa sasa.
|
|
0 Comments