📌BAHATI MSANJILA
Mfuko wa Taifa wa
Hifadhi ya Jamii (NSSF) umependekeza mabadiliko ya sheria ili kuwawezesha
wanachama waliopoteza ajira lakini hawana vigezo vya kulipwa mafao yao kupata
fedha zao ndani ya miezi mitatu badala ya kusubiri kwa muda mrefu.
Mkurugenzi Mkuu wa
NSSF, Masha Mshomba, akizungumza leo jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Taasisi
hiyo yaliyopatikana kwenye Serikali ya awamu ya sita amesa changamoto hiyo
imekuwa kero kwa wanufaika waliokuwa wakisubiri mafao yao kwa zaidi ya miezi
18, lakini sasa Serikali imetambua suala hilo na inaifanyia kazi ili kutoa
suluhisho la kudumu.
Mshomba amesema
Katika kipindi cha miaka minne, thamani ya mfuko imeongezeka kwa asilimia 92
kutoka Shilingi trilioni 4.8 mwezi Februari 2021 hadi Shilingi trilioni 9.3
mwezi Februari 2025. Mafanikio haya yametokana na kuongezeka kwa wanachama
wapya 1,052,176, kukua kwa vitegauchumi, na ongezeko la michango iliyokusanywa
kufikia Shilingi trilioni 6.9.
Aidha, NSSF
imeongeza kiwango cha mkupuo wa awali wa mafao ya kustaafu kutoka asilimia 25
hadi asilimia 35 na inatarajia kupandisha kiwango cha chini cha pensheni ya
kila mwezi kutoka Shilingi 100,000 hadi 150,000.
Katika kuboresha
huduma kwa wanachama, Mshimba ameeleza kuwa NSSF imewekeza katika TEHAMA,
ambapo matumizi yake yameongezeka kutoka asilimia 48 mwaka 2021 hadi asilimia
87.5 mwaka 2025, huku yakitarajiwa kufikia asilimia 100 ifikapo Juni 2025.
Mshomba amesema
mfuko huo utaendelea kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha
haki za wanachama zinalindwa, huku ukiboresha huduma na kuimarisha uwekezaji
wake ili kuhakikisha ustawi wa wanachama na mfuko kwa ujumla.
0 Comments