📌BAHATI MSANJILA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary
Senyamule, ameishukuru Benki ya NMB na Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania
(ALAT) kwa mchango wao katika kuendeleza maendeleo ya mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma ametoa shukrani hizo wakati akizungumza kwenye hafla ya Iftar
iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa wananchi wa mkoa wa Dodoma na wajumbe wa
ALAT.
Senyamule
amesema uwepo wa ALAT jijini Dodoma kwa siku tatu ni fursa kubwa kwa wakazi na
wafanyabiashara wa mkoa huo.
Amebainisha kuwa
ziara ya viongozi wa ALAT katika miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa
jijini Dodoma itawawezesha kueleza kwa Watanzania kazi kubwa inayofanywa na
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake,
Afisa wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Alfredy Shayo, amesema
hadi mwishoni mwa mwaka 2024, benki hiyo imefanikiwa kufikia vijiji 1,000
kupitia kampeni ya NMB Kijiji Day. Kampeni hiyo inalenga kuunga
mkono jitihada za serikali za kuhakikisha kila Mtanzania, popote alipo, anapata
huduma za kifedha, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi wa taifa na mtu mmoja
mmoja.
Shayo ameongeza
kuwa kwa mwaka 2025, NMB inapanga kufikia wananchi 2,000 ili kuwawezesha
kufungua akaunti ya NMB Pesa kwa gharama nafuu ya shilingi
1,000 pekee Akaunti hiyo inawapa wateja fursa ya kupata mikopo bila kulazimika
kufika katika matawi ya benki.
Katika kipindi
hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, Shayo amesema Benki ya NMB inatamani kutumia
mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kuombea uchaguzi wa amani.
Aidha, ametoa
wito kwa Jumuiya ya ALAT kushirikiana na NMB katika kutoa elimu ya kifedha kwa
wananchi.
Kwa niaba ya
wajumbe wa ALAT Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, White Zuberi,
ameishukuru NMB kwa kuwaunganisha katika hafla ya Iftar, akisema hatua hiyo
inaonesha umuhimu wa mshikamano na ushirikiano kati ya taasisi za kifedha na
viongozi wa serikali za mitaa.
Zuberi amesema
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewatia moyo kwa kutambua jitihada za baadhi ya
halmashauri katika kuwahudumia wananchi kwa niaba ya Serikali Kuu.
Amesema
kutambuliwa huko kunawapa nguvu zaidi ya kuendelea kuwatumikia wananchi kwa
uadilifu.
Akizungumza kwa
niaba ya Shekhe wa Mkoa wa Dodoma, Shehe Ahmad Said, ameombea dua kwa Mwenyezi
Mungu awabariki wote walioshiriki katika hafla ya Iftar na kuwajalia kila la
kheri Watanzania wote pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Samia Suluhu Hassan.
0 Comments