📌Na Mwandishi Wetu
Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT) kipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuanza kutoa
kozi ya urubani, ambapo Serikali imewekeza shilingi bilioni 6 kuhakikisha kozi
hiyo inakidhi viwango vya kimataifa.
Mkuu wa chuo hicho,
Dkt. Prosper Mgaya, amesema hayo wakati akizungumzia mafanikio ya NIT chini ya
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameeleza kuwa
chuo kinapaswa kupita hatua tano za kupata ithibati ya kimataifa, ambapo tayari
nne zimekamilika, na hatua ya mwisho inahusisha kuthibitishwa rasmi kwa utoaji
wa mafunzo hayo.
Kwa mujibu wa Dkt.
Mgaya, Tanzania imekuwa ikitumia fedha nyingi za kigeni kuwasomesha marubani
nje ya nchi, jambo linaloongeza gharama kwa wanafunzi na Serikali.
Hata hivyo,
kuanzishwa kwa kozi hiyo ndani ya NIT kutapunguza gharama za masomo kwa
asilimia 50 hadi 60, hatua ambayo itawawezesha Watanzania wengi kupata mafunzo
kwa urahisi zaidi.
Ameongeza kuwa
programu hiyo itachangia kuongeza idadi ya marubani wazawa na kupunguza
utegemezi wa marubani wa kigeni ambao hulipwa gharama kubwa.
Pia, itasaidia
kudhibiti changamoto ya marubani wa nje kutumia Tanzania kama sehemu ya
kuongeza masaa ya kuruka kabla ya kuhamia mashirika makubwa ya ndege.
Dkt. Mgaya
amesisitiza kuwa kuanzishwa kwa kozi hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha
sekta ya usafiri wa anga nchini.
0 Comments