📌BAHATI MSANJILA
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umefanikiwa kuokoa zaidi
ya shilingi bilioni 22 kutokana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA), hatua iliyodhibiti udanganyifu katika matumizi ya kadi za
bima.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, mfumo wa TEHAMA
umeimarisha uwajibikaji na uwazi, huku ukiwezesha wanachama kutambulika kwa
kutumia namba ya utambulisho wa Taifa (NIDA) badala ya kadi za bima.
Aidha,
matumizi ya TEHAMA yamerahisisha usajili wa wanachama, ambapo sasa mtu anaweza
kujiandikisha popote alipo bila kulazimika kufika ofisi za NHIF. Pia, huduma za
madai ya vituo vya afya sasa zinachakatwa kwa haraka zaidi, jambo ambalo
limeongeza ufanisi wa Mfuko.
Kutokana
na maboresho haya, NHIF sasa ina uwezo wa kujiendesha kwa mwaka mmoja na nusu,
tofauti na hapo awali ambapo Mfuko ulikuwa na uwezo wa kujiendesha kwa miezi
sita pekee.
Mbali
na udhibiti wa udanganyifu, NHIF pia imefanikiwa kupanua huduma zake kwa kiasi
kikubwa. Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mfuko
umesajili wanachama milioni 2.2 na kukusanya michango ya jumla ya shilingi
trilioni 2.3.
Dkt.
Isaka amebainisha kuwa asilimia 92 ya mapato hayo yanatokana na michango ya
wanachama, jambo linaloonesha jinsi wananchi wanavyoendelea kuamini na kutumia
huduma za NHIF.
Ili
kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zaidi, NHIF imeongeza idadi ya vituo
vya afya vinavyopokea kadi za bima hadi kufikia 14,000, vikiwemo vya Serikali
na sekta binafsi.
Dkt. Isaka amewahimiza wananchi, hususan vijana, kujisajili katika mfuko huo ili kuhakikisha wanapata huduma za afya kwa urahisi, akibainisha kuwa asilimia 22 ya vijana wanakabiliwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
0 Comments