MSD YASEMA UWEKEZAJI WA SERIKALI WAOKOA MAISHA YA MAMA NA MTOT

 



  📌BAHATI MSANJILA


MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai, amesema kupungua kwa vifo vya watoto wachanga na akina mama wakati wa kujifungua kumechangiwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya afya.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya MSD katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Tukai alisema kuwa vifo vya akina mama wakati wa kujifungua vimepungua kutoka 556 mwaka 2016/2017 hadi 104 mwaka 2021/2022.

 

Kwa mujibu wa Tukai, MSD imeshiriki katika kupunguza vifo vya mama na mtoto kupitia mradi wa SIMCO, uliolenga kuondoa athari za uzazi anazopata mama wakati wa kujifungua.

 

Akizungumzia upatikanaji wa bidhaa za afya, alisema MSD imeendelea kuimarisha huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa wakati.

 

Kwa mujibu wa Tukai, hali ya upatikanaji wa bidhaa hizo imeongezeka kutoka asilimia 42 mwaka 2021/2022 hadi asilimia 67 kufikia Februari 2024, sawa na ongezeko la asilimia 23.

 

Tukai alisema katika kipindi cha uongozi wa Awamu ya Sita, idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya vinavyohudumiwa na MSD imeongezeka kutoka 7,095 mwaka 2021/2022 hadi vituo 8,466 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la vituo 1,371 (asilimia 19).





Post a Comment

0 Comments