📌Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeendelea
kuimarisha usalama wa kemikali kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye
maghala ya kuhifadhi kemikali na maeneo ya mipaka ili kuhakikisha zinatumika
kwa mujibu wa sheria na hazileti madhara kwa binadamu na mazingira.
Akizungumza leo Machi 14, 2025, jijini Dodoma, Mkemia Mkuu wa
Serikali, Dkt. Fidelis Mafumiko, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya
Serikali ya Awamu ya Sita, mamlaka hiyo imefanya ukaguzi wa maghala 8,521, sawa
na asilimia 119 ya lengo la maghala 7,160, ikiwa ni hatua muhimu ya kudhibiti
kemikali hatarishi.
Aidha, amesema mamlaka imefanikiwa kudhibiti uingizaji na
usafirishaji wa kemikali kwa kutoa vibali maalum, ambapo idadi ya vibali vya
uingizaji imeongezeka kutoka 40,270 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 158,820
kufikia Desemba 2024, sawa na ongezeko la asilimia 294.
Ameeleza kuwa ongezeko hilo limechangiwa na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA, mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, pamoja na uelewa mkubwa wa wadau kuhusu sheria na kanuni za usimamizi wa kemikali.
0 Comments