📌Na Mwandishi Wetu
OFISI ya Makamu wa Rais imezikumbusha Wizara za
kisekta kuhusu wajibu walionao katika kufungamanisha taarifa za mazingira
wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ili kuharakisha ukuaji wa shughuli za
maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu
(Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi wakati akifungua
kikao kazi cha kukuza uelewa kwa wadau wa Wizara za kisekta kuhusu uandaaji wa
mfumo jumuishi wa usimamizi wa mazingira nchini.
Mitawi amesema mazingira ni sekta mtambuka
inayogusa Wizara zote za kisekta ndani ya Serikali na hivyo upo
umuhimu wa kuandaa mfumo jumuishi utakaorahisisha upatikanaji wa taarifa
zitakazosaidia taifa kubaini changamoto za mazingira na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.
Aidha Mitawi amesema Serikali kupitia Ofisi ya
Makamu wa Rais imekusudua kuanzisha mfumo huo wa ukusanyaji wa taarifa za
mazingira ikiwa ni hatua muhimu ya kurahisisha na kuimarisha sekta ya hifadhi
ya mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameongeza kuwa Wizara za kisekta zimekuwa
zikitekeleza majukumu mbalimbali kuhusu uhifadhi wa mazingira lakini
zimeshindwa kuwa na mfumo wa utambuzi na kusababisha ukosefu wa taarifa na
muhimu pindi zinapohitajika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya usimamizi
wa mazingira Sura 191 kifungu 175 Ofisi ya Makamu wa Rais, imepewa jukumu la
kusimamia mchakato wa ukusanyaji wa taarifa za mazingira nchini ambazo zimekuwa
zikitumika katika majukwaa na mikutano mbalimbali ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Mitawi amesema uandaaji wa mfumo
jumuishi utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza hapo awali
kuhusiana na upatikanaji wa taarifa za mazingira, na hivyo kuzitaka Wizara za
kisekta kutoa ushauri, maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha mfumo
huo.
Kwa upande Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya
Makamu wa Rais, Dkt. Paul Deogratius amesema mfumo huo umekuja kwa wakati
mwafaka kwani utawezesha taarifa mbalimbali za mbalimbali katika Wizara za
kisekta kuweza kusomana na hivyo kusaidia katika mipango ya maendeleo.
Amesema kuwa Serikali imekuwa ikifanya kazi nzuri
kuhusu masuala ya uhifadhi wa mazingira lakini zimeshindwa kuripotiwa na
kuonekana kutokana na ukosefu wa mfumo sahihi wa utunzaji na uhifadhi wa
taarifa hizo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Ofisi ya Makamu wa
Rais Bi. Joyce Mnunguli amesema Ofisi hiyo imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika
kukamilisha mfumo huo ambao utasaidia kujibu changamoto mbalimbali za ukosefu
wa taarifa za mazingira nchini
0 Comments