📌BAHATI MASANJILA
SERIKALI ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza miradi
mikubwa ya maji ili kuhakikisha wakazi wa Dar es Salaam wanapata huduma bora na
ya uhakika ambapo miradi kadhaa imeanzishwa na mingine inaendelea
kukamilika, lengo likiwa ni kuongeza upatikanaji wa maji safi katika jiji hilo
lenye wakazi wengi.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa
DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema kuwa juhudi kubwa zinaendelea kufanyika
ili kupanua huduma za maji kwa wananchi.
Miongoni mwa miradi
inayotekelezwa ni ule wa Mkuranga Awamu ya Pili, unaolenga kusambaza maji
katika maeneo kama Dundani, Mwanambaya, Kisemvule, Vikindu, Mwandege, na Kipara
Mpakani.
Miradi mingine inayolenga
kuboresha hali ya upatikanaji wa maji ni ule wa Kazimzumbwi, ambao utahudumia
wakazi wa Kifuru, Msimbu, Homboza, Kitanga, na maeneo mengine yaliyo pembezoni
mwa jiji.
Amesema Pia, Mradi wa Mama Samia Industrial
Park unaendelea kutekelezwa ili kuhakikisha maeneo ya Disunyara, Kilangalanga,
Kisabi, Mhande, na Mlandizi yanapata maji safi ya uhakika.
Ameongeza kuwa Kwa sasa huduma ya maji safi
jijini Dar es Salaam imefikia asilimia 45, huku mipango ya muda mfupi na mrefu
ikiwa ni kupanua mtandao wa maji ili kuwafikia wakazi wengi zaidi.
Mbali na huduma za maji safi, mamlaka hiyo pia
inatekeleza miradi mbalimbali ya majitaka ili kuhakikisha mazingira yanabaki
safi na salama kwa wakazi wa jiji hilo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Bwire, miradi kadhaa ya
usafi wa mazingira imekamilika, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo vya umma
katika wilaya zote za Dar es Salaam, hatua inayolenga kupunguza uchafuzi wa
mazingira.
Aidha, miradi mikubwa ya kuchakata majitaka
inaendelea, ikiwemo ule wa Mbezi Beach, unaohusisha ulazaji wa bomba la
kilomita 101 kwa gharama ya Shilingi bilioni 132.2.
Amesema Utekelezaji wa mfumo wa majitaka
katika maeneo ya Mbezi Juu, Mbezi Chini, Kilongawima, na Salasala tayari
umefikia asilimia 57.25, huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2026.
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita,
DAWASA imefanikiwa kutekeleza miradi 25 yenye thamani ya Shilingi bilioni
987.6. Kati ya miradi hiyo, ile ya thamani ya Shilingi bilioni 232.9 tayari
inatoa huduma kwa wananchi, huku mingine yenye thamani ya Shilingi bilioni
754.7 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mhandisi Bwire amesema kuwa mamlaka hiyo pia
imeanza utekelezaji wa bwawa la Kidunda kwa gharama ya Shilingi bilioni 335.9,
ambalo litaongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam. Hadi sasa,
zaidi ya Shilingi bilioni 85.4 zimetolewa kwa ajili ya mradi huo, na ujenzi
wake umefikia asilimia 28.
Serikali pia imeidhinisha maandalizi ya mradi
mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji, ambao utahakikisha mahitaji ya maji
jijini Dar es Salaam yanatosheleza hadi mwaka 2050.
Kwa mujibu wa Mhandisi Bwire, hatua ya kuandaa
michoro ya mwisho na nyaraka za manunuzi ya mradi huo tayari imefikia asilimia
89.
0 Comments