MIFUMO YA KIDIJITALI YALETA MAGEUZI KATIKA USIMAMIZI WA MBOLEA



  📌BAHATI MSANJILA

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesema kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali yameleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, hususan katika usimamizi wa mbolea na takwimu muhimu kwa wakulima. 

Akizungumza jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent,ameeza kuwa mifumo hii imeimarisha utoaji wa huduma, udhibiti wa ubora wa mbolea, na kurahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi zinazosaidia Serikali kupanga maendeleo ya sekta ya kilimo.

Kwa mujibu wa TFRA, kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huu, wakulima walilazimika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa mbolea kwa bei ya juu. Hata hivyo, kupitia ruzuku inayosimamiwa kidijitali, wakulima sasa wanaweza kupata mbolea kwa bei elekezi

Mbali na kupunguza gharama, mfumo wa kidijitali umeimarisha uwazi na ufuatiliaji wa mbolea kuanzia kiwandani hadi kwa mkulima, na hivyo kusaidia kudhibiti udanganyifu katika sekta hiyo. 

Katika hatua nyingine, TFRA imeeleza kuwa matumizi ya mifumo ya TEHAMA yamepunguza muda wa kupata leseni na vibali vya biashara ya mbolea kutoka siku 14 hadi siku mbili pekee. 

Kwa mujibu wa TFRA, matumizi ya mbolea nchini yameongezeka kutoka tani 363,599 mwaka 2020/2021 hadi tani 840,714 mwaka 2023/2024, huku lengo likiwa kufikia tani milioni moja ifikapo 2030.

Pamoja na mafanikio hayo, TFRA imeweka vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwemo kuimarisha usambazaji wa mbolea kwa wakati, kuendelea kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea, na kuongeza uwekezaji katika viwanda vya uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi ili kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje.





Post a Comment

0 Comments