📌Na Mwandisi Wetu
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Halima Mdee, amewataka Watumishi wa Umma na Viongozi kutekeleza wajibu wao kwa ufasaha ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Mdee akizungumza katika ziara ya Kamati
hiyo kukagua miradi mbalimbali ya afya na elimu inayotekelezwa Halmashauri ya
Kyela, mkoani Mbeya, amesema Kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa wakati na kwa
ufasaha, viongozi hawatakuwa na haja ya kuja kukagua.
Ameeleza kuwa kutokana na ukubwa wa nchi,
haiwezekani kwa kiongozi mmoja kutembelea kila mahali kutoa huduma, hivyo
majukumu hayo yamekabidhiwa kwa Watumishi wa Umma ili kuhakikisha wananchi
wanapata huduma stahiki.
Aidha, amewataka Watumishi wa Umma kutekeleza
maelekezo yanayotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge na kuhakikisha wanazitatua
dosari zinazobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
kwa kutoa taarifa sahihi.
Naye, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI,
Mhe. Dkt. Festo Dugange, amesema Ofisi yake imechukua maelekezo yote
yaliyotolewa na Kamati na itayasimamia kikamilifu katika utekelezaji wake.
Pia, Mhe. Dkt. Dugange amewataka Watumishi wa
Umma kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika
ipasavyo ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuzingatia thamani ya fedha.
0 Comments