COSOTA YAONGEZA NGUVU KATIKA USIMAMIZI WA HAKIMILIKI

 



    📌BAHATI MSANJILA

Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imepiga hatua katika kuimarisha usimamizi wa hakimiliki, kuhakikisha wasanii na waandishi wanapata haki zao stahiki kupitia mirabaha na tozo za hakimiliki.

 

Akizingumza waandishi wa habari  jijini Dodoma Mtendaji Mkuu wa COSOTA, Doreen Senare, amesema taasisi hiyo imefanikiwa kuanzisha vyanzo vipya vya mapato kwa wabunifu kupitia marekebisho ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na. 7 ya mwaka 1999.


 Miongoni mwa mabadiliko makubwa ni kuanzishwa kwa tozo ya hakimiliki (copyright levy) inayotozwa kwa vifaa vinavyotumika kusambaza, kuzalisha na kuhifadhi kazi za sanaa na fasihi. Kuanzia Septemba 2023 hadi Februari 2025, COSOTA imekusanya jumla ya shilingi bilioni 1.4 kupitia chanzo hiki.

 

Katika kuhakikisha usambazaji wa mirabaha unakuwa wa haki na uwazi, COSOTA imeruhusu uanzishwaji wa Makampuni ya Wasanii ya kukusanya na kugawa mirabaha (CMOs), huku taasisi hiyo ikibaki kuwa msimamizi. Tayari kampuni ya Tanzania Music Rights Society (TAMRISO) imepewa leseni ya kukusanya mirabaha ya muziki, na hadi Novemba 2024 ilikuwa imekusanya shilingi milioni 256 kupitia baa, hoteli, na maeneo mengine ya biashara.

 

Aidha, idadi ya kazi za sanaa na fasihi zilizosajiliwa imeongezeka kwa asilimia 70 tangu mwaka 2021, huku zaidi ya kazi 11,500 na wabunifu 3,436 wakisajiliwa. COSOTA pia imeongeza juhudi za elimu ya hakimiliki kwa wasanii na waandishi kupitia semina, midahalo, na programu za redio na televisheni.

 

Katika kuhakikisha Tanzania inanufaika na mikataba ya kimataifa ya hakimiliki, COSOTA imekuwa ikihamasisha kuridhiwa kwa Itifaki ya Beijing na Mikataba ya WIPO kuhusu Hakimiliki ya Mtandaoni. Hatua hizi zinatarajiwa kuboresha mazingira ya ulinzi wa kazi za sanaa na fasihi, pamoja na kuongeza mapato kwa wabunifu nchini.

 

Kwa miaka minne ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, COSOTA imeendelea kufanya mageuzi makubwa, ikijidhatiti kuboresha mifumo ya usajili, usimamizi wa mirabaha, na kutoa elimu kwa wadau wa hakimiliki nchini.

 

Senare amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, taasisi hiyo imepokea na kushughulikia migogoro 136 ya hakimiliki, ongezeko kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na wastani wa migogoro 3 au 4 kwa mwaka.

 

Senare amesema kupitia migogoro hiyo, wasanii wameweza kujifunza umuhimu wa kufuatilia haki zao na kuhakikisha wanasaini mikataba inayowalinda kwa kipindi na hadi miaka 50 baada ya vifo vyao.

 

Amesema mapato yaliyotokana na tozo ya haki miliki yatasaidia kuimarisha ulinzi wa haki za wasanii, kulipa mirabaha, na kuongeza ufanisi wa usimamizi wa hakimiliki nchini.

 

Senare amesema taasisi hiyo imeshirikiana na wadau wa Singeli kwa kuwasajili wasanii na nyimbo zao, ili kuhakikisha wanapata haki zao za mirabaha na kunufaika na kazi zao.

 

COSOTA inaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha wasanii wa sekta zote wanalindwa kupitia sheria za hakimiliki, huku ikiimarisha mifumo ya usajili, usimamizi wa mirabaha, na utoaji wa elimu kuhusu haki zao.

 



Post a Comment

0 Comments