📌BAHATI MSANJILA
Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA),
Mhandisi Justine Rujomba, amesema mamlaka hiyo imeendelea kuboresha upatikanaji
wa majisafi na huduma za majitaka kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa
ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB).
Akizungumza jijini
Dodoma katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO kuhusu mafanikio ya AUWSA
katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mhandisi Rujomba amesema mradi
mkubwa wa maji wenye thamani ya Shilingi bilioni 520 umekamilika kwa lengo la
kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira kwa wakazi wa Arusha.
Aidha, amesema
mradi wa majisafi wa Oldonyosambu unaogharimu Shilingi bilioni 6.3, ambao
utahudumia wakazi wapatao 29,449 katika vijiji vya Oldonyosambu, Lemanda,
Lemong’o, Oldonyowasi na Lesinoni, umefikia asilimia 50 ya utekelezaji.
Katika juhudi za
kupanua huduma za maji, AUWSA pia inatekeleza mradi wa kuboresha usambazaji wa
maji katika Kata za Baraa, Moivaro, na Moshono kwa kujenga mtandao mpya kutoka
visima vya Shangarai hadi tanki la majisafi Moshono One.
Mradi huu
unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji kwa lita milioni 5 kwa siku.
Kwa mwaka wa fedha
2024/25, upatikanaji wa majisafi jijini Arusha umefikia asilimia 99 kupitia
mradi mkubwa wa usambazaji maji, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya serikali ya
kuhakikisha wakazi wa mijini wanapata maji safi na salama kwa asilimia 95
ifikapo 2025.
Mhandisi Rujomba
amebainisha kuwa AUWSA imejipanga kuendelea kutekeleza miradi kwa ufanisi na
kushirikiana na serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha huduma za
majisafi na usafi wa mazingira zinaboreshwa kwa maendeleo endelevu ya Jiji la
Arusha na maeneo ya jirani.
0 Comments