BILIONI 25.7 ZAWEKEZWA KUBORESHA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UBUNIFU

 



📌BAHATI MSANJILA


Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, amesema serikali imewekeza Shilingi bilioni 25.7 katika utafiti, ubunifu, na maendeleo ya teknolojia katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, hatua inayolenga kuimarisha sekta ya sayansi na teknolojia nchini.

 

Akizungumza jijini Dodoma, Dkt. Nungu amesema kupitia uwekezaji huo, COSTECH imefadhili zaidi ya tafiti 50 katika sekta za elimu, kilimo, afya, na mazingira, huku vituo vya ubunifu 111 vikiimarishwa ili kuleta suluhisho la kisayansi kwa jamii. 

 

Dkt Nungu amesema Matokeo ya uwekezaji huu ni usajili wa kampuni mpya 70 zinazotokana na wabunifu waliowezeshwa na serikali.

 

Aidha, serikali imetenga Shilingi bilioni 6.3 kwa ajili ya miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na Shilingi milioni 600 kwa miradi minne ya usalama wa chakula, ikiwemo udhibiti wa magonjwa ya mazao na uboreshaji wa uhifadhi wa chakula. 

 

Pia, kupitia Samia Commercialization Fund, Shilingi bilioni 2.3 zimetolewa kusaidia wabunifu wa Kitanzania kuingiza bunifu zao sokoni, hatua inayosaidia kuondoa changamoto ya mitaji kwa wabunifu.

 

Katika kuhakikisha Tanzania inabaki kwenye ushindani wa kimataifa, COSTECH imeanzisha kongano nane bunifu katika mikoa mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuboresha sekta ya viwanda na kilimo kwa kutumia teknolojia.








Post a Comment

0 Comments