UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU YAONGEZA UFANISI WA USAFIRI NCHINI

 




📌BAHATI MSANJILA

Wakala ya Barabara Tanzania (TANRODS) imesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, kumekuwa na mafanikio makubwa katika sekta ya ujenzi, hususan kwenye miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege.


Tangu mwaka 2021, hali ya miundombinu ya barabara nchini imeimarika kutoka asilimia 88 hadi asilimia 90, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Akizungumza jijini Dodoma kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa TANRODS, Mhandisi Ephatar Mlavi, amesema serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege na madaraja kwa lengo la kuimarisha usafiri na kuchochea maendeleo.

Amesema wakala huo unatekeleza jumla ya miradi 38 katika mikoa 17 nchini, ambapo miradi ya viwanja vya ndege na madaraja tisa imekamilika huku barabara zenye urefu wa kilomita 15,625 zikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Hata hivyo, Mlavi amesema ushiriki wa makandarasi wazawa, washauri elekezi na wanawake katika miradi ya matengenezo ni wa kuridhisha, lakini bado kuna changamoto katika ushiriki wao kwenye miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara kuu na barabara za mikoa.

Ameeleza kuwa baadhi ya changamoto zinazosababisha hali hiyo ni makandarasi kutoa bei za chini kupita kiasi katika zabuni, changamoto za weledi, uwajibikaji na uaminifu, mazingira magumu ya upatikanaji wa mitaji, ucheleweshaji wa malipo bila riba ya ucheleweshaji, pamoja na fursa za upendeleo kwa kampuni za wazawa kutozaa matunda yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuelekea kutimiza miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, Idara ya Habari (MAELEZO) imejipanga kuwafahamisha wananchi kuhusu mafanikio yaliyopatikana.

Ameeleza kuwa serikali imejidhatiti kuimarisha sekta ya usafiri wa umma kwa kuongeza mabasi yaendayo haraka 150 pamoja na kushirikiana na sekta binafsi kuboresha usafiri wa mijini.

Amesisitiza kuwa taasisi zote za serikali zinapaswa kufuata ratiba zilizopangwa kwa kutoa taarifa kwa wananchi, na taasisi yoyote ambayo haitafanya hivyo itapaswa kutoa maelezo ya kutokutekeleza jukumu hilo.





Post a Comment

0 Comments