📌BAHATI MSANJILA
Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA) inatekeleza miradi 10 ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa Bandari mpya ya Mbegani
wilayani Bagamoyo, utakaogharimu Dola za Kimarekani bilioni 1.5. Miradi hii
inalenga kuboresha miundombinu na kuongeza ufanisi wa bandari nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, amesema miradi
hiyo inatekelezwa chini ya Mpango
Kabambe wa Maendeleo ya Bandari (2020–2045) na Programu ya Uboreshaji na Uendeshaji wa Bandari, iliyosajiliwa mwaka 2023 kwa namba ya mradi 4,300.
Amesema ushirikishwaji wa sekta binafsi umeongeza ufanisi,
ambapo mapato yamepanda kutoka wastani wa Shilingi bilioni 850 kwa mwezi mwaka
2023/24 hadi Shilingi trilioni 1 kwa mwezi mwaka 2024/25.
Kwa mujibu wa TPA, kiasi cha shehena kinachohudumiwa
kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 15.23 kwa mwaka, kutoka tani milioni 20.78
mwaka wa fedha 2021/22 hadi tani milioni 27.55 mwaka wa fedha 2023/24.
Vile vile ametaja miradi mingine kuwa
ni Ujenzi wa kituo cha reli na mtandao wake ndani ya bandari ya Dar es Salaam
na unagharimu dola za kimarekani million 119.955 ambao umelenga kupunguza
kiwango cha asilimia 98 cha shehena inayotoka bandarini na ujenzi wa bandari
maalum ya kisiwa - mgao mkoani Mtwara kwa ajili ya kuhudumia shehena chafu na
utagharimu dola za kimarekani million 171.
Amesema mradi huo umelenga kuepusha
athari za kimazingira na kuondoa changamoto zinazotokana na kuhudumia mizigo
hiyo katika bandari ya Mtwara.
Mbossa pia ametaja miradi mingine
kuwa ni Ujenzi wa gati namba 12 hadi 15 utakao gharimu dola za kimarekani
million 591.564 unaolenga kuongeza ufanisi wa bandari ya DSM na ujenzi wa
bandari mpya ya Mbegani Bagamoyo utakao gharimu dola za kimarekani billion 1.5.
Amesema miradi hiyo ya kimkakati
itakapokamilika italeta manufaa mbalimbali ikiwemo mchango katika Makusanyo ya
Mapato ya Nchi.
Kadhalika amesema,Mamlaka hiyo
imekuwa na mchango katika Ajira Nchini ambapo sekta hiyo huchangia katika kutoa
ajira za moja kwa moja kwa kuwa Taasisi za umma na Binafsi zinazofanya kazi
Bandarini zimeajiri watumishi wanaotoa huduma Bandarini.
Aidha, katika mwaka wa fedha wa
2022/23 mchango wa sekta ya bandari ulikuwa Shilingi trilioni 10.8 sawa na
asilimia 7.3 ya pato la Taifa lililokuwa Shilingi trilioni 148.3.
TPA inasimamia
bandari rasmi 131 zilizoko Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu, ikiwa na majukumu
makuu kama kuendeleza bandari, kushirikisha sekta binafsi, na kusimamia
uendeshaji wa shughuli za bandari.
0 Comments