📌BAHATI MSANJILA
Naibu
Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Khamis Hamza
Khamis, amesema kuwa jumla ya miti milioni 686.24 iliyopandwa katika
halmashauri mbalimbali nchini imestawi, sawa na asilimia 82.3 ya miti yote
milioni 866.7 iliyopandwa kati ya mwaka 2020/2021 hadi 2023/2024.
Mhe. Khamis ametoa taarifa hiyo Februari 5, 2025,
bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe.
Tunza Malapo alietaka kufahamu iwapo tathmini imefanyika ili kubaini miti
inayopandwa, kutunzwa, na kukua kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi.
Ameeleza kuwa tathmini ya upandaji wa miti
hufanyika kila mwaka kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI ili kupambana
na uharibifu wa ardhi, ukame, na kuenea kwa hali ya jangwa hivyo Kwa msimu wa
mwaka 2024/2025, tathmini inaendelea kufanyika ili kubaini idadi ya miti
iliyopandwa na iliyostawi kote nchini.
Aidha, Mhe. Khamis amesisitiza umuhimu wa
kushirikisha wananchi na sekta binafsi katika kampeni za upandaji wa miti ili
kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kutunza mazingira.
Ametoa wito kwa Watanzania kutumia mvua
zinazonyesha kipindi hiki kupanda miti katika maeneo mbalimbali.
Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Tunza Malapo kuhusu
mkakati wa kuhakikisha miti inatunzwa, Mhe. Khamis amesema kuwa Ofisi ya Makamu
wa Rais ina maafisa viungo katika mikoa yote ya Tanzania Bara wanaosimamia na
kufuatilia utekelezaji wa zoezi la upandaji miti.
Vilevile, ameeleza kuwa kampeni mbalimbali zimeanzishwa
ili kuhamasisha upandaji wa miti katika vyanzo vya maji, mashuleni, na pia
matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya
kuni na mkaa.
0 Comments