📌BAHATI MSANJILA
Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kudhibiti madhara ya mmomonyoko wa ardhi na kupanuka kwa kingo za mito, ikiwemo Mto Mpiji wilayani Bagamoyo, mkoa wa Pwani.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis, amesema hayo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Bagamoyo, Mhe. Muharami Mkenge, ambaye alitaka kufahamu lini Serikali itajenga kingo za Mto Mpiji zilizopanuka kutokana na mvua kubwa na kuhatarisha makazi ya wananchi.
Mhe. Khamis amesema kuwa Serikali imechukua hatua kadhaa kudhibiti athari za mmomonyoko wa kingo za mito, ikiwa ni pamoja na kuandaa Mwongozo wa Usafishaji wa Mito ili kuondoa mchanga na tope.
Ameeleza kuwa kikosi kazi maalum
kimeundwa kushughulikia usafishaji wa mito kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira,
Sura ya 191, kifungu cha 57 (2), ambacho kimempa Waziri mamlaka ya kutunga
kanuni ndogo na mwongozo wa usimamizi wa mazingira.
Amwsema Katika juhudi za kudhibiti athari za mvua, Serikali inatumia njia za asili kwa kupanda miche 5,000 ya michikichi, migomba, miti maji, na matete katika kingo za mto kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 100 katika Kata ya Mabwepande, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Pia, Serikali imeweka utaratibu
maalumu wa uondoaji wa mchanga kwa kuunda vikundi 12 vya wapakia mchanga na
wakandarasi 14 wa uchimbaji wa mchanga kwa mfumo wa kusafisha mto ili kuruhusu utiririshaji wa maji kwa njia ya asili.
Mhe. Khamis amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali kupitia Wizara ya Maji imepanga kutenga shilingi milioni 552 kwa ajili ya ujenzi wa kingo za Mto Mpiji.
Ujenzi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika mwaka huo wa fedha ili kuhakikisha usalama wa makazi ya wananchi na kupunguza madhara ya mafuriko.
0 Comments