Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025, Mwenyekiti wa Kamati Mhe, Timotheo Mnzava, amesema migogoro ya ardhi imeendelea kuwa changamoto kubwa, hasa katika Jiji la Dodoma, licha ya juhudi zilizochukuliwa.
Kamati hiyo imesema migogoro mingi inasababishwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uendelezaji wa mji bila fidia kwa wananchi, urasimishaji wa makazi usio wa uwazi, na uadilifu duni wa watumishi wa sekta ya ardhi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mnzava, amesema kuwa pamoja na juhudi zilizochukuliwa, bado Dodoma inaendelea kuwa moja ya maeneo yenye migogoro mingi ya ardhi nchini.
Amesema baadhi ya miradi mikubwa kama Uwanja wa Mpira wa Nala, barabara ya mzunguko (Ring Road), na Reli ya Mwendo Kasi (SGR) imechukua ardhi ya wananchi bila kulipa fidia stahiki, jambo linalosababisha malalamiko makubwa.
Mnzava amesema kamati imebaini kuwa moja ya sababu kubwa za migogoro hiyo ni watumishi wa sekta ya ardhi wasio waaminifu, ambao wanadaiwa kushirikiana na walanguzi wa ardhi kufanya upangaji wa umiliki wa viwanja mara mbili na kuchelewesha huduma kwa makusudi ili kushinikiza utoaji wa rushwa.
Akizungumzia juhudi zilizofanyika, amesema kuwa serikali ilianzisha Kampeni ya Zero Migogoro Jiji la Dodoma mwaka 2021, ikaunda Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi mwaka 2022, na kuendesha Kliniki za Ardhi mwaka 2023 lakini juhudi hizo bado hazijamaliza kabisa changamoto hiyo, kwani malalamiko kutoka kwa wananchi yanaendelea.
Kamati hiyo imependekeza kuwa serikali ibuni njia za kudumu za utatuzi wa migogoro ya ardhi ili sekta hiyo iweze kuchangia ipasavyo katika pato la taifa.
Pia, imeitaka serikali kuongeza uhamasishaji wa wananchi kuhusu ulipaji wa kodi za ardhi na kutoa elimu ya matumizi bora ya ardhi ili kuondoa mkanganyiko unaosababisha migogoro.
Akichangia taarifa iliyowasilishwa Mhe. Angeline Mabula Mbunge wa Ilemela ameiomba serikali kuangalia swala la kugatua madaraka kwenye swala la usimamizi wa ardhi kwakuweka wakala atakaefanya kazi nzuri kama wanavyofanya Tarula na Maji kwasababu serikali ilishatoa wakala wa haraka wakufanya kazi hiyo.
Nae Mbunge wa Nyasa Eng. Stella Manyanya amesema swala la mazingira ni swala mtambuka na lipo kila Wizara na linapokuwa halina chombo madhubuti lakusimamia linakuwa haliendi vizuri hivyo amesisitiza kuwa ni vyema kuwa na chombo madhubuti chakusimamia mazingira na wataalamu wa mazingira wawe na bodi yao.
0 Comments