📌BAHATI MSANJILA
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka
majaji na mahakimu kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa haki, kwa kuzingatia
makubaliano ya kisheria na kikatiba, badala ya kujiona kama miungu watu.
Rais Samia ameyasema hayo Februari 3, 2025, wakati wa kilele cha
Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, yaliyofanyika katika Viwanja vya
Chinangali jijini Dodoma amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo
inadhihirisha dhamira ya kuifanya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuwa na
mipango madhubuti ya kukuza haki nchini.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa dira hiyo hautakuwa rahisi, hivyo
ni muhimu kwa Mahakama na wadau wake kuanza kujipanga kwa umakini ili
kuhakikisha haki inapatikana kwa ufanisi zaidi.
Akizungumzia usimamizi wa haki jinai na haki madai amesema kuwa
kaulimbiu ya mwaka huu isemayo Tanzania
ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki katika Kufikia Malengo Makuu ya
Dira ya Taifa ya Maendeleo.” inampa faraja kwa sababu
inadhihirisha kuwa agizo lake alilolitoa kuhusu uboreshaji wa taasisi za haki
jinai linaendelea kufanyiwa kazi.
Aidha, amesema kuwa Serikali imeendelea kuiwezesha Tume ya
Utumishi wa Mahakama kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Amebainisha kuwa serikali inatambua kuwa katika kazi kuna haki
na wajibu, na ndiyo maana imekuwa ikisisitiza wajibu wa mahakama na taasisi za
haki jinai na haki madai katika kuimarisha ustawi wa jamii na haki nchini.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma,
amesema kuwa maadhimisho haya hutumika kuwaombea watoa haki na kuwakumbusha
kuwa kazi yao ni utume wa Mungu, hivyo wanapaswa kutenda haki kwa uadilifu.
Ameeleza kuwa wananchi waliopata elimu hiyo wamewasilisha maoni
mbalimbali, ambayo ni mtaji muhimu wa kujipima, kujitathmini, na kuweka
mikakati thabiti ya kuboresha huduma za utoaji haki.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amesema kuwa ofisi
yake inaamini kuwa kupitia ushirikiano wa wananchi na taasisi husika, mafanikio
makubwa yatafikiwa katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na kwa usawa.
Ameongeza kuwa mfumo wa haki utakuwa nguzo muhimu katika
kufanikisha Tanzania yenye misingi imara ya haki na usawa, kwa mujibu wa Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),
Boniface Mwakabusi, amesema kuwa ushirikiano kati ya chama hicho na Serikali si
dalili ya kupewa upendeleo, bali ni utekelezaji wa wajibu wa pamoja wa
kuhudumia wananchi.
Ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuwapatia gari
litakalowasaidia kuwafikia wananchi kwa urahisi. Amesema kuwa TLS ipo tayari
kupokea msaada wowote kutoka kwa mtu au taasisi yoyote kwa lengo la kuimarisha
upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria ni tukio muhimu linalotoa fursa
kwa wadau wa sekta ya sheria kujadili changamoto na mafanikio katika mfumo wa
utoaji wa haki nchini.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini Tanzania kwa
mwaka 2025 ni: “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki katika
Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”
0 Comments