📌BAHATI MSANJILA
Serikali
inaendelea kuimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuliwezesha kwa vitendea
kazi muhimu, ikiwemo ununuzi wa magari 150 ya kisasa ya kuzima moto na uokoaji,
pamoja na vifaa vingine vinavyohitajika.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent
Bashungwa,amebainisha hayo tarehe 3 Februari 2025 alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Shangai, aliyetaka kufahamu lini Serikali
itanunua gari la zimamoto kwa ajili ya Wilaya ya Ngorongoro.
“Kwa sasa, Serikali inatekeleza mradi wa ununuzi
wa vifaa mbalimbali vya kuzima moto na uokoaji, ikiwemo magari 150 ya zimamoto
ambayo yatakapowasili nchini, yatasambazwa kote nchini, ikiwemo Wilaya ya
Ngorongoro,” amesema Bashungwa.
Aidha, Waziri huyo amefafanua kuwa Serikali ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imewezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
kupata magari 12 ya kisasa, ambapo moja lilitumiwa kwa mafanikio kuzima moto
katika jengo la TRA Kariakoo.
Mbali na hilo, Bashungwa amebainisha kuwa Serikali
ina mpango wa kununua helikopta maalum kwa ajili ya Jeshi la Zimamoto na
Uokoaji ili kuongeza ufanisi katika operesheni za uokoaji na kudhibiti majanga
ya moto.
Pamoja na hilo, maafisa, wakaguzi na askari wa
jeshi hilo wataendelea kupatiwa mafunzo maalum ili kuongeza ujuzi wao katika
kukabiliana na dharura.
Hatua hizi ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa
kuhakikisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linakuwa na uwezo wa kutekeleza
majukumu yake kwa ufanisi zaidi katika kukabiliana na majanga ya moto na
uokoaji wa wananchi kote nchini.
0 Comments