📌BAHATI MSANJILA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji
ya Umma (PIC) imeeleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa na Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), katika kusimiamia utekelezaji wa ujenzi wa minara
758 inayojengwa katika kata 713 nchini licha ya changamoto za ubovu wa barabara
zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo, utekelezaji wa mradi huo umefikia
asilimia 52.4.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Mhe. Augustine Holle (Mb), baada ya kamati kutembelea na kukagua ujenzi wa
minara katika kata ya Esilalei na Sepeko, wilayani Monduli, mkoani Arusha,
ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa uwekezaji huo unakuwa wenye tija.
Mhe. Holle ameongeza kuwa, licha ya mafanikio
hayo UCSAF ina wajibu wa kuendelea kusimamia na kufanya ufuatiliaji kwani
maelekezo ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa watoa
huduma wanakamilisha ujenzi wa minara yote ifikapo Mei 13, 2025 kama ilivyo
ilivyoainishwa katika mikataba, na kuwa Serikali haitaongeza muda wa
utekelezaji wa mradi huo.
“Tunajua maelekezo ya Rais ni kuwa mradi huu
hautaongezewa muda, na sisi kama Kamati tunapenda kusisitiza hapo, wasimamieni
watoa huduma wakamilishe kwa wakati ili tija ya uwekezaji huu uonekane kwa
wananchi kwa kuanza kupata mawasiliano” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa UCSAF,
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utafiti Mhandisi Albert Richard amesema, kupitia
mradi huo jumla ya minara 141 inajengwa katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini
ambayo ni Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Manyara.
Naye mkazi wa kijiji cha Sepeko, Letema Saning’o
amesema kabla ya kuanza kupata mawasiliano walikuwa wakiteseka kwa kutembea
umbali mrefu kufuata mtandao, lakini sasa anaishukuru Serikali kwani tangu
mnara huu uanze kutoa huduma hawana tena uchangamoto ya mawasiliano. Kwa upande
wake Kadogo Maenga, mkazi wa Esilalei, amesema kwa sasa hawatafuti tena mbinu
mbadala za kupata mawasiliano tangu mnara huo ulipoanza kutoa huduma.
Serikali kupitia UCSAF imetoa ruzuku ya shilingi
bilioni 126 kwa makampuni ya simu kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu ili
kufikisha mawasiliano kwa wananchi wapatao milioni 8.5. Hadi sasa Serikali
imeshalipa kiasi cha shilingi bilioni 70 ili kuwezesha watoa huduma kuagiza vifaa
vya ujenzi wa minara kwa kuwa asilimia kubwa ya vifaa huagizwa nje ya nchi.
0 Comments