📌BAHATI MSANJILA
Tanzania
inaendelea kung’ara katika huduma za matibabu ya moyo kupitia Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI), ambayo imepiga hatua kubwa katika miaka minne ya
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt.
Peter Kisenge, taasisi hiyo imefanikiwa kuwahudumia wagonjwa zaidi ya 745,000,
huku baadhi ya wagonjwa wakitoka mataifa mbalimbali barani Afrika na hata nje
ya bara hili.
Dkt. Kisenge amesema Mbali na kuhudumia wagonjwa
wa ndani, JKCI imekuwa kitovu cha matibabu ya moyo kwa Afrika Mashariki na
Kati, ikipokea wagonjwa 689 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Somalia, Kenya,
Rwanda, Malawi, Msumbiji, na hata nje ya Afrika, ikiwemo Ujerumani, China,
India, na Uingereza.
Pia, wataalamu wa JKCI walivuka mipaka na kutoa
huduma katika Malawi, Zambia, na Jamhuri ya Watu wa Comoro, ambako walihudumia
wagonjwa 1,189 na kutoa rufaa kwa wagonjwa 262 waliokuwa wakihitaji matibabu ya
kibingwa Tanzania.
Amesema JKCI imeweza kufanya upasuaji wa moyo kwa
njia mpya zisizo na maumivu makali, ikiwa ni pamoja na upasuaji wa moyo wa
kutumia tundu dogo bila kufungua kifua, pamoja na teknolojia ya kisasa ya
Cathlab inayowezesha kuzibua mishipa ya damu ya moyo kwa usahihi mkubwa.
Wagonjwa wapatao 8,789 wamepata matibabu haya ya
kisasa, huku 469 wakifanyiwa matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo.
Aidha, taasisi hiyo imefanikiwa kupunguza rufaa za
matibabu nje ya nchi kwa Watanzania kwa zaidi ya asilimia 90, huku ikihamasisha
utalii wa tiba kwa kuwahudumia wagonjwa 689 kutoka nchi mbalimbali kama
Nigeria, Malawi na Msumbiji.
Ameongeza kuwa Serikali imewekeza shilingi bilioni
2.16 kuboresha huduma za wagonjwa mahututi, kuongeza vitanda katika ICU, na
kujenga miundombinu ya kisasa kama jengo la ghorofa nne la utawala na vipimo
pamoja na mitambo ya kuzalisha hewa ya oksijeni yenye thamani ya zaidi ya
bilioni 1.8.
Dkt. Kisenge amesisitiza kuwa mafanikio haya
yamewezekana kutokana na msaada wa Serikali, uwekezaji katika teknolojia, na
kujitoa kwa wataalamu wa JKCI.
0 Comments