📌BAHATI MSANJILA
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekemea tabia
ya baadhi ya wanachama wa Chama hicho wakiwemo Wabunge kuanza kufanya
kampeni chafu zenye nia ya kuchafuana wenyewe kwa wenyewe
kabla ya uchaguzi nakusisitiza kuwa wagombea watapimwa kwa sifa, tabia na
uwezo wa kukubalika katika jamii badala ya nguvu ya fedha.
Katibu Mkuu wa CCM na mgombea mwenza wa kiti cha
urais, Dkt. Emmanuel Nchimbi amekemea tabia hiyo leo jijini Dodoma wakati
akifungua mafunzo ya Watendaji wa Kata na Makatibu wa Matawi Mkoa wa Dodoma,
amesisitiza kuwa mfumo mpya wa upigaji kura umeongeza idadi ya wapiga kura kwa
asilimia 900 ili kuondoa rushwa na kupima wagombea kwa maendeleo badala ya
fedha.
Katika hotuba yake, Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa
ushindi wa chama unatokana na uimara wake, utendaji wa viongozi, na utekelezaji
wa ilani ya chama.
Amesema chama kinapaswa kujengwa kwa misingi
ya uadilifu na si kwa kuzingatia kiwango cha fedha cha mgombea.
Kwa mujibu wake, kabla ya mgombea
kupitishwa, atapimwa kwa sifa, tabia, na uwezo wa kukubalika katika jamii, Dkt.
Nchimbi ameonya kuwa ni kosa kubwa la kimaadili kupuuza Katiba na kanuni za
chama.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakipitisha fomu
kwa wanachama na viongozi kwa njia zisizo halali ili mgombea apitishwe bila
kupingwa Amewataka waache mara moja tabia hiyo, akisisitiza kuwa yeyote
atakayebainika ataondolewa kwenye orodha ya wagombea.
Aidha, amebainisha kuwa wanachama wote wana haki
ya kugombea nafasi za uongozi, na kwamba juhudi zozote za kuwashawishi wajumbe
waache kupinga mgombea fulani zitapelekea wahusika kuenguliwa.
Katibu Mkuu huyo pia ameonya kuhusu tabia ya
wanachama kufanya shughuli za kifamilia na kualika wajumbe kwa malipo ili kupata
kura. Amesema taarifa za watu wa aina hiyo zipo na hatua kali zitachukuliwa
dhidi yao.
Amesema Rushwa imepata jeraha la kudumu kutokana
na mfumo huu, na wanachama pamoja na wagombea wachapakazi wamefurahi kwa kuwa
wanapata nafasi ya kutumikia wananchi.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma Pili
Agustino amesema mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama na
yatawasaidia watendaji wa kata na makatibu wa matawi kufanya kazi yao kwa
ufanisi zaidi.
Naye Katibu wa NEC Organization Issa Gavu, amesema
mafunzo haya ni muendelezo wa maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM, yakisisitiza kuwa
chama huanzia mashinani, ambako ndiko kuna wanachama na wapiga kura. Amewataka
washiriki wa mafunzo hayo kuyazingatia kwa umakini ili yawe na manufaa makubwa
kwa chama na jamii kwa ujumla.
Jumla ya washiriki 274 wanahudhuria mafunzo haya,
wakitarajiwa kuimarisha uongozi wa chama katika ngazi za kata na matawi ili
kuhakikisha ushindi wa CCM unapatikana kwa misingi ya uadilifu, ushawishi na
maendeleo.
0 Comments