Wajumbe wa Bodi ya Wakala wa Vipimo (WMA)
wametembelea jengo jipya la Makao Makuu ya wakala huo na kumwagiza mkandarasi
kuhakikisha anakamilisha kazi na kukabidhi rasmi jengo hilo ifikapo Februari 10
mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua
hatua za ujenzi wa jengo hilo Mwenyekiti wa Bodi ya WMA Prof. Eliza
Mwakasungura, amesema wajumbe wa Bodi wameridhishwa na maendeleo ya ujenzi
baada ya kukagua jengo hilo lenye ghorofa tano huku wakielekeza marekebisho
madogo yaliyosalia, kama upakaji rangi, yakamilike kabla ya tarehe ya
makabidhiano.
“Nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Shilingi
bilioni 6.2 kwa ajili ya ujenzi huu. Pia, nampongeza Waziri wa Viwanda na
Biashara, Mheshimiwa Jafo, pamoja na menejimenti yake kwa usimamizi mzuri wa
mradi huu,” alisema Prof. Mwakasungura.
Kwa upande wake,Mtendaji Mkuu wa WMA,Alban Kihulla amesema
ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 97 na tayari mkandarasi amepewa fedha
yote Sh bilioni 6.2.
“Tuna hakika kazi iliyobaki itakamilika kwa wakati.
Kukamilika kwa jengo hili kutasaidia kutatua changamoto ya majengo kwa Makao
Makuu na Ofisi ya Mkoa, kwani sasa wote watakuwa hapa,” alisema Kihulla.
Kwa upande wake, Mkandarasi wa jengo hilo, Mohammed Jafferji
wa kampuni ya Mohammed Builders, amethibitisha kuwa kazi inaendelea na
wanajitahidi kuhakikisha wanakabidhi jengo hilo kwa muda uliopangwa.
“Kufikia Februari 10 tunatarajia kuwa tumemaliza kazi zote
zilizobaki, tukishirikiana na mshauri elekezi ili kuhakikisha kila kitu kipo
sawa,” alisema Jafferji.
Jengo hili jipya linatarajiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa
Wakala wa Vipimo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma zake.
0 Comments