BMT YAWEKA WAZI MAFANIKIO YA MIAKA MINNE KATIKA SEKTA YA MICHEZO

 



📌BAHATI MSANJILA

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya michezo ndani ya kipindi cha miaka minne, akisisitiza mchango mkubwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhamasisha na kuboresha mazingira ya michezo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Msitha alisema kuwa katika kipindi hicho, kumekuwa na ongezeko kubwa la ufadhili, ujenzi wa miundombinu ya kisasa na ushirikiano wa kimataifa, hatua ambazo zimechangia mafanikio makubwa katika sekta ya michezo.

Miongoni mwa miradi ya miundombinu iliyotekelezwa ni ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa uliogharimu shilingi bilioni 31, ujenzi wa uwanja mpya wa michezo jijini Arusha wenye gharama ya shilingi bilioni 338, pamoja na ujenzi wa uwanja mpya wa michezo Dodoma utakaogharimu shilingi bilioni 310. Pia, serikali imewekeza shilingi bilioni 21 katika ujenzi wa viwanja vya mazoezi kama Gymkhana, Leaders Club, TIRDO, Law School na uwanja wa Farasi.

Msitha alieleza kuwa Tanzania imefanikiwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa Kanda ya Nne wa kupinga matumizi ya dawa na mbinu haramu michezoni, uliofanyika Dar es Salaam mwezi Novemba 2024. Aidha, serikali imeondoa kodi ya nyasi bandia, hatua ambayo imechochea ujenzi wa viwanja vingi katika ngazi za halmashauri na kuongeza ushiriki wa vijana katika michezo.

Katika hatua nyingine, Tanzania imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, wenye lengo la kusaidia timu za taifa, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa michezo, kuboresha miundombinu, kununua vifaa vya michezo na kuendeleza vipaji. Kupitia mfuko huu, Tanzania ilifanikiwa kushiriki Kombe la Dunia la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu na Kombe la Dunia la mpira wa miguu kwa wanawake chini ya miaka 17, yaliyofanyika India mwaka 2022. 

Kwa upande wa maendeleo ya vilabu, mfumo wa usajili wa kidijitali umeongeza idadi ya vyama vya michezo vilivyosajiliwa kutoka 368 hadi kufikia vyama 1,638 ndani ya kipindi cha miaka minne.

Mchezo wa mpira wa miguu umeendelea kung’ara, ambapo hamasa ya Goli la Mama imesaidia timu za Simba na Yanga, pamoja na timu za taifa, kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali. Katika mchezo wa gofu kwa wanawake, Tanzania ilishinda mashindano ya All Africa Challenge Trophy mwaka 2022, huku mchezo wa riadha ukileta heshima kwa nchi kwa kuandaa mashindano ya vijana ya ukanda wa Afrika Mashariki chini ya miaka 18 na 21 (EARR), ambapo Tanzania ilimaliza katika nafasi ya pili na ya tatu.

Mafanikio pia yameonekana katika mchezo wa Kriketi, ambapo mwaka 2024, Tanzania ilishinda mashindano ya ICC Men’s T20 World Cup Sub Regional Africa Qualifier na ICC U-19 World Cup Qualifier Africa Division 2.

Kwa upande wa michezo ya watu wenye ulemavu, Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na mchezo wa tenisi ya viti mwendo na mpira wa miguu kwa wenye ulemavu.

Baraza la Michezo la Taifa limeahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa michezo nchini ili kuhakikisha sekta hiyo inazidi kuimarika na kuiletea nchi mafanikio zaidi katika anga za kimataifa.





 

 


Post a Comment

0 Comments