📌BAHATI MSANJILA
Katika juhudi za kukuza utalii wa kihistoria nchini, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limeanzisha kipindi maalum kuhusiana na msafara wa watumwa (The Slave Caravan) kupitia Tanzania Safari Channel chenye kuelezea historia ya njia zilizotumiwa na watumwa kusafirisha mizigo ya wakoloni kutoka Zanzibar kupitia Bagamoyo hadi Ujiji mkoani Tabora.
Hatua hii inalenga kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea maeneo haya yenye historia ya kipekee.
Akizungumza leo Alhamisi, Januari 23, 2025, Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk. Ayub Rioba, amesema kuwa utafiti wa kina uliofanywa kwa kushirikiana na wataalamu wa historia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) umebaini kuwa njia hii ya kihistoria bado inapitika kwa aina mbalimbali za usafiri kama vile miguu, baiskeli, pikipiki na magari.
Njia hii ya kihistoria siyo tu inatoa fursa ya kujifunza kuhusu historia ya watumwa, bali pia inatoa nafasi ya kufurahia mandhari ya kipekee ya Tanzania. Hii ni moja ya juhudi za kufanikisha maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kampeni ya Tanzania Royal Tour,
Kwa mujibu wa Dk. Rioba, njia hii ya kati
inaanzia Ujiji mkoani Tabora, ambako watumwa walibebeshwa mizigo ya meno ya
tembo na kupelekwa Bagamoyo kabla ya kusafirishwa kwa mashua kwenda Zanzibar.
Alama za kihistoria kama majengo ya kale, miti iliyotumika kupumzikia na
kunyongea watumwa, bado zinapatikana katika baadhi ya maeneo ya njia hiyo.
Akizungumza kuhusu utunzaji wa maeneo hayo ya
historia Dk. Rioba amesema kipindi hiko kitasaidia kizazi cha sasa na vijavyo
kujifunza mambo yaliyotokea kipindi cha historia nakutokuruhusu kurudi kwenye
utumwa.
Mtaalamu wa historia kutoka UDSM, Salvatory
Nyanto, ameongeza kuwa kulikuwa na njia tatu kuu za biashara ya watumwa nchini
Tanzania—njia ya kati (Tabora hadi Zanzibar), njia ya kusini (Kilwa hadi
Mauritius kupitia Zanzibar), na njia ya kaskazini (Tanga kupitia Pangani hadi
kwa Wamaasai).
Hii ni hatua muhimu kwa TBC katika kuendeleza
urithi wa kihistoria wa Tanzania na kuhamasisha utalii unaoendana na kuhifadhi
kumbukumbu za historia ya nchi.
0 Comments