📌BAHATI MSANJILA
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith
Kapinga, kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko, ametoa ufafanuzi kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme maeneo ya
vijijini, akieleza kuwa wananchi wa vijijini wanapaswa kulipia shilingi 27,000/-,
huku wale wa vijiji mji wakitakiwa kulipa shilingi 320,960/-.
Mhe. Kapinga
ameyasema hayo leo Januari 30, 2024, bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu
swali la Mbunge wa Bukene, Mhe. Selemani Zedi, aliyetaka kufahamu kwa nini
wakazi wa Bukene na Itobo hawaunganishiwi umeme kwa gharama ya shilingi
27,000/-.
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Bukene na Itobo ni vijiji mji, hivyo gharama ya kuunganisha umeme inakuwa shilingi 320,960/- kwa mujibu wa utaratibu wa serikali,” amesema Mhe. Kapinga.
Amebainisha kuwa
serikali inaendelea kufanya tathmini kuona kama kuna uwezekano wa kuboresha
gharama hizo kulingana na tathmini zilizofanyika. Pia, ameeleza kuwa amemuagiza
Meneja wa Mkoa wa Tabora na Meneja wa Wilaya ya Nzega kufanya tathmini ya kina
ili kupata majibu sahihi kuhusu maeneo hayo na kuondoa mkanganyiko uliopo.
Katika hatua
nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakari Asenga, kuhusu
kwa nini wakazi wa Katinduka wanalipia shilingi 320,960/- licha
ya kuwa kijijini, Mhe. Kapinga amesema gharama ya shilingi 27,000/- inahusu
maeneo yaliyotambuliwa rasmi kama vijiji na ambayo yamepata ufadhili wa miradi
ya umeme vijijini. Ameeleza kuwa siyo kila eneo linakidhi vigezo hivyo,
na kwamba Katinduka ni sehemu ya mtaa, hivyo gharama yake ni
tofauti.
Kwa upande
mwingine, Mhe. Kapinga amejibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Anatropia
Theonest, kuhusu upatikanaji wa umeme katika vijiji vya Buganza na Nyarigongo
wilayani Kyerwa. Amesema umeme umeshafika katika makao makuu ya vijiji hivyo,
na kwamba mkandarasi anaendelea na kazi ya kusambaza umeme katika kilometa
mbili za ziada ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Serikali
imeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kufahamu tofauti ya maeneo ya vijiji
na vijiji mji ili kuepusha mkanganyiko kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme,
huku ikiahidi kuendelea kufanya maboresho kulingana na tathmini zinazoendelea
kufanyika.
0 Comments