SERIKALI YATOA MSIMAMO KUHUSU KUCHELEWESHWA KWA MAITI HOSPITALINI

 




📌BAHATI MSANJILA

Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu madai ya maiti kuzuiliwa hospitalini kutokana na deni la matibabu, ikisisitiza kuwa suala hilo si jukumu la madaktari bali ni la uongozi wa hospitali husika.

Akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Mhe. Bonna Ladislaus Kamoli, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa katika ufuatiliaji uliofanywa ili kuchukua hatua za kinidhamu, imebainika kuwa mara nyingi ndugu wa marehemu hukataa kufuata utaratibu uliowekwa, jambo linalochangia ucheleweshaji wa kutoa miili.

Aidha ameeleza kuwa baadhi ya ndugu huchagua kulalamika kwa vyombo vya habari na viongozi badala ya kushughulikia taratibu zinazopaswa kufuatwa.

Ameongeza kuwa Serikali imeeleza kuwa tayari imetoa waraka namba moja wa mwaka 2021 unaoelekeza kutoruhusu maiti kuzuiliwa hospitalini kwa sababu ya madeni ya matibabu.

Dkt. Mollel amesema Waraka huo umeweka utaratibu wa kulipa gharama hizo bila kuathiri utoaji wa huduma kwa wafiwa.

Amesisitiza kuwa Serikali inasimamia utekelezaji wa miongozo hiyo ili kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa, huku akihimiza ndugu wa marehemu kushirikiana na uongozi wa hospitali kufuata taratibu zinazostahili.





Post a Comment

0 Comments