📌BAHATI MSANJILA
Takwimu za Serikali kwa
mwaka 2024 zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya wanawake na wasichana wameathirika
kutokana na utoaji mimba usio salama, ambapo 181,071 walihitaji huduma katika
vituo vya afya na kuhudumiwa kama wagonjwa wa nje, huku 32,512 walilazwa
hospitalini kwa ajili ya matibabu zaidi kutokana na matatizo ya kuharibika kwa
mimba.
Aidha, takwimu zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2022
hadi 2024, wanawake 92 walipoteza maisha kutokana na matatizo mbalimbali
yaliyosababishwa na kuharibika kwa mimba.
Akijibu swali la Mhe. Fatma Hassan Toufiq Mbunge
Viti Maalum) Leo Bungeni Jijini Dodoma Naibu Waziri wa Afya mhe. Godwin Mollel
ameeleza kuwa changamoto za utoaji mimba usio salama zinaathiri afya ya
wanawake na wasichana, na kwamba Serikali inatambua umuhimu wa kutoa huduma
bora za afya ya uzazi.
Ameeleza kuwa katika juhudi za kupunguza athari za
utoaji mimba usio salama, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya ya uzazi
na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatari zinazohusiana na utoaji mimba katika
mazingira yasiyo salama.
Waziri huyo amesisitiza kuwa takwimu hizi
zinapaswa kuchukuliwa kama kengele ya tahadhari kwa jamii na Serikali, ili
kuhamasisha watu kuchukua hatua za tahadhari na kufuata mifumo sahihi ya uzazi,
ikiwa ni pamoja na kutafuta huduma bora za afya wakati wa matatizo ya uzazi.
Serikali pia inaendelea kutoa maelekezo kwa vituo
vya afya kuhusu utoaji wa huduma za dharura na kutoa elimu ya afya kwa jamii
ili kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na utoaji mimba usio salama.
Katika mwaka 2022, Serikali ilitangaza kuwa
inasimamia kwa karibu utekelezaji wa sera na mipango ya afya ya uzazi, ikiwa ni
pamoja na kutoa huduma kwa wanawake na wasichana walioathirika na utoaji mimba
Hata hivyo bado kuna changamoto kubwa ya wanawake wengi kutafuta huduma hizi
kwa kuchelewa, jambo linaloathiri matokeo ya afya yao.
Serikali imesisitiza kuwa, licha ya changamoto
hizo, itaendelea kutekeleza mikakati ya kupunguza athari za utoaji mimba usio
salama, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi na
kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa huduma za afya ya uzazi.
0 Comments