📌BAHATI MSANJILA
NAIBU Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan
Chande, ameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka mfumo madhubuti wa
ununuzi wa umma kwa kutumia wataalam wa ndani, akisisitiza umuhimu wa kusimamia
kwa ufanisi fedha za Serikali zinazotumika katika ununuzi.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa mazungumzo na
Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, iliyotembelea Mamlaka ya
Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa lengo la kujifunza masuala ya ununuzi, Mhe. Chande
alisema kuwa mfumo bora wa ununuzi siyo tu utarahisisha michakato, bali pia
utaongeza uwazi na kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana.
“Zaidi ya asilimia 70 ya bajeti zetu hutumika
kwenye ununuzi wa umma. Kwa hiyo, tunapojadili Muswada wa Sheria ya Ununuzi, ni
lazima tuhakikishe sheria inakuwa thabiti ili kuondoa changamoto zinazoweza
kujitokeza,” alisisitiza Mhe. Chande.
Aidha, aliipongeza Kamati hiyo kwa kuchukua hatua
ya kuja kujifunza katika PPRA kabla ya kupitisha Muswada wa Sheria ya Ununuzi
wa Umma unaotarajiwa kujadiliwa katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Pia,
aliwataka kuendelea kushirikiana na PPRA kwa kutembelea mifumo iliyoimarika,
ikiwemo mfumo wa ununuzi uliowekwa jijini Arusha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya
Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mwanaasha Khamis Juma, alisema kuwa hatua
ya kuja kujifunza ni muhimu kwa kuwa kamati hiyo inawajibika kuhakikisha fedha
za Serikali zinatumika kwa tija.
“Kamati yetu inahusika moja kwa moja na kupitisha
bajeti ya Serikali ambayo ndani yake kuna miradi mikubwa. Tumekuja kujifunza
kutoka kwa wenzetu wa PPRA kuhusu sheria, taratibu na changamoto zinazohusu
ununuzi.
0 Comments